Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mtwara aagiza kampeni upimaji Ukimwi kufanyika kwa miezi sita

12479 PIC+UKIMWI TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Katika kutekeleza kampeni ya upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU), mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ameziagiza halmashauri zote mkoani hapa kufanya kampeni ya uhamasishaji miezi sita mfululizo, kuanza upimaji kila penye mkusanyiko wa watu.

Byakanwa alitoa agizo hilo leo Ijumaa Agosti 17, 2018 katika  uzinduzi wa kampeni ya ‘furaha yangu’ ambayo hotuba yake iliyosomwa  na mkuu wa Wilaya ya Mtwara,  Evod Mmanda na kusema kwa kufanya hivyo kutapunza kiwango cha maambukizi ya VVU  kutoka asilimia mbili iliyopo kwa sasa.

“Kwa mkoa na halmashauri zote kwa kushirikiana na wananchi na wadau wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri zote wanaagizwa kusimamia kampeni hii kwa uzito unaotakiwa,” amesema Mmanda.

Mratibu wa mradi huo kutoka Taasisi ya Mkapa, Dk Rose Kaaya alisema mango huo unalenga kuwafikia  zaidi ya watu 2,000 katika kila kata ambazo zimeingizwa kwenye kampeni.

“Kwa Mtwara mradi utatekelezwa katika Wilaya ya Masasi na Mtwara , tukiwa na melengo ya kufikia kata zote ambapo tutafanya upimaji katika ngazi ya jamii na madhumuni ni kufikia wilaya nane na kata 184 katika mikoa ya Arusha, Tanga, Manyara na Mtwara,”amesema Kaaya.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Renatus Macalius amesema upimaji wa VVU utaendelea katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya mkoani humo kila siku.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye kampeni hiyo wameipongeza Serikali kwa kuanzisha kampeni hiyo na kutoa wito kwa watu kujitokeza na kupima afya zao.

“Nitoe pongezi nyingi na shukrani kwa waziri mkuu aliyeanzisha jambo hili na kuitikiwa katika ngazi za mkoa na taasisi mbalimbali, kilichobaki sasa ni zamu ya wananhi kujitokeza kwa wingi,”amesema Kunyengana Njohoka.

Hamza Hamis amesema: “Jamii hususani wanaume wenzangu wasiwe waoga wajitokeze kwa wingi kupima afya zao,wakipima watakuwa wanajitambua.”

Chanzo: mwananchi.co.tz