Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi kuwaona watu wakishirikiana na kushikamana kwa pamoja kwa kuendekeza fitina na majungu.
RC Mtanda amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Butiama katika fainali za tamasha la michezo na ujasiriamali lilifanyika katika Viwanja vya Mwenge Wilayani humo na kudhaminiwa na Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini,
Mtanda amesema kuwa penye maendeleo lazima pawe na mshikamano kama aliouonesha Mhe. Sagini kupitia tamasha la michezo la "Sagini Cup 2023" na amesema michezo ni sehemu ambayo huwaleta watu wa marika yote mahali pamoja na jamii yenye umoja na mshikamano maendeleo lazima yaonekane kwani wananchi pamoja na viongozi wote wanakuwa wameshikamana na wanazungumza lugha moja.
"Leo nimekuja kwa tukio maalumu la kushiriki michezo iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Butiama.Wilaya ya Butiama ndipo Wilaya aliyozikwa Baba wa Taifa hili Hayati Mwl.Nyerere ni Wilaya muhimu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika miezi iliyopita pale Wananchi walipopata changamoto ya suala la Usalama tulishirikiana kwa pamoja mpaka wahalifu wote wakapatikana na sasa wapo kwenye vyombo vya kisheria.Tutaendelea kushikamana kwa pamoja na Butiama itaendelea kuwa salama masaa ishirini na nne"Alisema Mtanda.
Awali Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini alisema kuwa lengo la kuanzisha na kudhamini tamasha hilo ni kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kwa kuwaleta watu wa rika mbalimbali pamoja, kuibua vipaji mbalimbali katika jamii na kuona namna ya kuweza kuviendeleza vipaji hivyo katika ngazi za Kitaifa na Kimataifa.
Katika tamasha hilo lililohusisha mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kuendesha baiskeli na vikundi vya sanaa washindi katika michezo hiyo walijipatia zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu, makombe ya ushindi, medali na vifaa vya michezo.