Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mtaka awahakikishia wawekezaji mazingira rafiki

D6ca5210acfd6657575ead5cc05ab491.jpeg RC Mtaka awahakikishia wawekezaji mazingira rafiki

Wed, 8 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amesema wataendelea kuhakikisha Dodoma inakuwa mkoa wa kwanza wenye unafuu kiuwekezaji.

Alisema hayo jana jijini hapa wakati alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa Kiwanda cha mbolea cha Intracom kinachojengwa eneo la uwekezaji Nala jijini hapa.

Kiwanda hicho kinachojengwa na mwekezaji kutoka Burundi kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 180.

Mtaka alisema wataendelea kuhakikisha Dodoma inakuwa mkoa wa kwanza wenye unafuu kiuwekezaji nchini.

“Mtu ana fedha zake aje kuwekeza Dodoma ili Mji wa Dodoma ushamiri na kukua, tutabeba dhamana ya kuwaondolea wawekezaji urasimu kwenye ofisi za serikali tutaenda wenyewe kupanga foleni,” alisema.

Alisema eneo la ekari 3,000 limetengwa kwa ajili ya uwekezaji kwenye eneo la viwanda.

“Ekari 3,000 zimepimwa mtu mwenye fedha afike ili afahamu taratibu, pia unaweza kuingia ubia na serikali au jiji kwa ajili ya uwekezaji,” alisema.

Pia alitaka kuangaliwa kwa uwiano na raia wa kigeni wanaofanya kazi za ujenzi na wazawa, ambapo awali alielezwa kwamba kuna wafanyakazi 500 wakiwemo raia wa Burundi 200.

“Suala hilo liangaliwe kwani sheria iko wazi, pia suala la vibarua kufukuzwa kiholela lifanyiwe kazi, Mkuu wa Wilaya alikuja hapa Ijumaa (wiki iliyopita) na kuna taarifa vibarua 30 walifukuzwa ikiwemo wale waliouliza maswali, jambo kama hili si jema,” alisema.

“Kuna uhuru sana wa kuulizana, huo ndio utamaduni wetu, mnatakiwa mjifunze pia katika hili la utamaduni wa kuuliza maswali,” alisema.

Pia alimtaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuona namna ya kupanua barabara zote za eneo hilo kutokana na wenye kiwanda hicho hivi karibuni watahitaji kupitisha makontena 200 yenye mashine kwa ajili ya kufunga kiwandani hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, aliwataka vibarua kufanya kazi kwa bidii.

“Kazi ndio msingi wa kile kinachofanyika hapa, hakuna haki bila wajibu, kwa zile changamoto zilizojitokeza zitafanyiwa kazi,” alisema.

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, aliwataka vibarua wanaofanya kazi za ujenzi kujiamini na uongozi wa kiwanda ufikirie kuwapatia motisha ikiwemo vyeti na uwekwe utaratibu wa kuwa na msemaji

Meneja wa mradi, Musafiri Dieudorine, alisema mradi huo ulianza Julai mosi mwaka huu. Wana vibarua 500 na kati ya hao 200 ni raia wa Burundi ambapo hufanya kazi ya kujenga, kuchanganya zege na kunyanyua matofali.

Alisema wafanyakazi walioondolewa kazini ni waliokiuka taratibu za kazi na si kama walifukuzwa kutokana na kuuliza maswali.

“Wote wana vibali, walipewa viza za biashara na sasa tumeomba vibali vya kufanya kazi na kuishi, lakini tuko tayari kutekeleza maagizo ya serikali,” alisema.

Ofisa Mipango Miji wa Jiji la Dodoma, Aisha Masanja, alisema kiwanda hicho kitakuwa kikizalisha kemikali na mbolea na eneo zima la kiwanda ni ekari 21.3.

Alisema eneo zima la uwekezaji la Nala lina takribani ekari 3,000.

“Bado viwanja vipo, wanaohitaji kuja kuwekeza wachangamkie fursa, tuna viwanja kwa ajili ya viwanda vyenye ukubwa tofauti, kuna ekari 200, ekari 50, ekari 20 na viwanja vya ekari moja moja kwa ajili ya viwanda vya kutoa huduma kama mafundi magari,” alisema na kuongeza kuwa bei ya mita moja ya mraba ni Sh 5,000.

Chanzo: www.habarileo.co.tz