Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Morogoro apiga marufuku vibanda vya video, beti na vigodoro

33297 PIC+MORO Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amepiga marufuku uwepo wa vibanda vya kuonyesha video, mashine za kubeti (maarufu mashine za kichina) pamoja na ngoma za vigodoro.

Dk Kebwe ametoa uamuzi huo leo Jumatatu Desemba 24,2018 baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu kwa vigodoro, kubeti na vibanda vya video vimekuwa vikichangia kukithiri kwa utoro shuleni.

Amesema kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya maeneo wilayani vigodoro kukesha na kufanya mambo yasiyofaa katika jamii jambo linaloathiri watoto na hata kuwafanya wanafunzi kuchelewa kulala.

Kutokana na hilo, Dk Kebwe amewaagiza wakuu wa wilaya kama wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kuhakikisha wanasimamia na kutokuwepo kwa vitu hivyo huku akiwataka wazazi kutokuwa chanzo cha uvunjifu wa maadili katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amewakemea baadhi ya walimu kuweka rekodi utoro kwa watoto wa kike kwa kivuli cha kufisha suala la uwepo wa mimba.

Amesema tatizo la kuwepo mimba kwa mkoa wa Morogoro bado ni kubwa na limekuwa likiongezeka kila mwaka, ambapo kwa mwaka 2016 mimba zilikuwa 320 na 2018 zimeongezeka na kufikia 537 na kwa shule za msingi ni zaidi ya 100 wamekuwa wakipata ujauzito.

Pia amewataka wakuu wa wilaya kuwakama bila kuoneana aya watuhumiwa wote wanaohusika huku akitumia vyombo vya sheria ambapo ametoa  maagizo kwa viongozi wa elimu wilaya mpaka Machi 2019 awe ameona mchanganuo wa namna changamoto zilivyotatuliwa.

“Hivi vitu ndio vinavyosababisha watoto wetu kupata mimba, kutoroka shule na hata kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa, kama wazazi lazima tukemee kwa nguvu zetu,” amesema

Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali akichangia katika kikao hicho amesema katika wilaya yake amekuwa akikemea  hasa suala la vigodoro, lakini changamoto iliyopo ni hasa kipindi cha mavuno na hata baadhi ya wazazi kubadilisha mtindo wa sherehe wakijifanya ni harusi ama kipaimara.

Naye ofisa elimu Mkoa wa Morogoro, Joyce Baravuga amemuhakikishia mkuu wa mkoa wameendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na kupambana na tatizo la mimba kwa kujenga mabweni.

“Watoto wa kike tunaendelea kuwaelimisha namna ya kujikinga, wajiepushe pamoja na kuacha kurubuniwa na watu wasiokuwa wema kwao kwa kutodanganyika, pamoja na hayo jamii zitumie muda mingi kuzungumza na watoto wao,” amesema Baravuga.



Chanzo: mwananchi.co.tz