Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Morogoro agawa vitambulisho, atoa angalizo

32613 RCPIC Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amewataka wakuu wa wilaya za mkoa huo kusimamia ipasavyo ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara ili viwafikie walengwa.

Akizungumza katika uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo leo Alhamisi Desemba 20, 2018 katika chuo cha ualimu Kigurunyembe, Dk Kebwe amesema wakuu hao wa wilaya ndio wasimamizi katika maeneo yao, wanapaswa kuviona vitambulisho hivyo kama kaa la moto.

“Msimamie kwa mujibu wa maelekezo na taratibu zilizopo ili kuongeza mapato ya mkoa wetu kwa kuwa tumeonekana kushuka ikilinganishwa na mwaka 2017,” amesema Kebwe.

Ametaka vitambulisho hivyo kutolewa kwa uwazi na fedha zitakazopatikana baada ya wafanyabiashara kuvichukua, zisiiingie katika mfuko wa mtu binafsi.

“Mkoa umepatiwa vitambulishi 25,000 na vikiuzwa vyote tutapata Sh500milioni hii itatupandisha zaidi,” amesema.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo manispaa ya Morogoro, Faustin Francis akizungumza kwa niaba ya wenzake amesema wapo tayari kuchangia pato la Serikali kwa kuwa awali walikuwa wakishindwa kutokana na kusumbuliwa na mgambo.

“Natoa angalizo kwa wafanyabiashara wakubwa wasitumie mwanya wowote kwa sababu vitambulisho hivi ni vya wafanyabiashara wadogo, kwa sasa tunaanza kutambuana sisi wenyewe,” amesema.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz