Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mongella azitaka taasisi za elimu kusisitiza somo la historia

Mongela Arusha RC Mongella azitaka taasisi za elimu kusisitiza somo la historia

Thu, 9 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), John Mongella amezitaka taasisi za elimu nchini kusisitiza somo la historia shuleni ikiwa ni pamoja na Serikali kutoa kipaumbele kuenzi historia mbalimbali za nchi.

Ameyasema hayo leo Desemba 8, 2021 katika viwanja vya makumbusho ya Azimio la Arusha wakati wa kusheherekea siku ya kumbukumbu ya miaka 60 ya uhuru.

Mongella amesema kuwa ni wakati wa walimu kusisitiza somo la historia mashuleni ili wanafunzi wajue walipo na walipotoka kwani wengi hawajui historia, hivyo kuwataka walimu kuweka mkazo zaidi kwenye somo hilo.

"Ni lazima tuyaenzi na kuyaendeleza yale yote yaliyoandaliwa na waasisi wetu kwani mengi hayajapitwa na wakati na nawaombeni sana tuendelee kushikamana na kuwa kitu kimoja, huku tukihakikisha kila mtu anatoka na lengo la miaka 60 ya Uhuru na tujipange kwa maendeleo makubwa yanayokuja kwa ajili yetu."amesema.

Mongella amesema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha wanaenzi mambo mbalimbali yaliyoachwa na waasisi wetu ikiwemo amani, mshikamano pamoja na utengamano wa Taifa letu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa makumbusho ya Azimio la Arusha, Dk Gwakisa Kamatula amewataka Watanzania kujijengea utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali hususani katika jumba la makumbusho la kihistoria Ili kujifunza mambo mbalimbali ya kale.

Amesema kuwa tunapozungumzia miaka 60 ya Uhuru ni kitovu cha historia ya nchi yetu,hivyo tunapaswa kuyaenzi yale yote yaliyoanzishwa ikiwemo kudumisha Uhuru, amani na mshikamano miongoni mwetu .

Naye Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Martin Ngoga amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuyatunza na kuyaenzi yale yote yaliyoanzishwa katika miaka 60 ya Uhuru na tusione ni kitu cha kawaida bali tuzidi kuyaendeleza kwa ajili ya vizazi na vizazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live