Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mongella awataka Wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati

RC MONGELA.jpeg RC Mongella awataka Wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati

Tue, 16 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo inayohusu kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Mongella amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kampeni hiyo iliyoanza Juni 15, Mwaka huu, huku akisisitiza wafanyabiashara kulipa kipaumbele suala la ulipaji kodi kwa wakati ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma jamii.

“Kama mnavyojua umuhimu wa kodi na hasa katika kipindi hiki cha awamu ya tano hakuna mtanzania ambaye hajashuhudia umuhimu wa kodi, tumeona barabara zikijengwa, ndege zikinunuliwa, ujenzi wa vituo vya afya, meli zikijengwa, ukarabati wa viwanja vya ndege ambavyo vyote vimesababishwa na uwezo wa serikali ambao umejengeka kwa mapato ya ndani,” amesema Mongella.

Aidha, Mongella ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TRA pindi wanapopita katika maeneo yao ya biashara, na pia kupitia hao maafisa wataweza kupata elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati na hata kujua haki zao.

Amesema zoezi hilo limelenga kuwafikia wananchi na Wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali mkoani humo ikiwamo Rwagasore, Pamba Road, Buhongwa, Nyerere Road, Misungwi, Mwaloni na Kisesa.

Sambamba na hayo amesema mambo yote yamefanikiwa kutokana na uadilifu na utendaji kazi wenye tija uliofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kusimamia mapato ya ndani na kuyaelekeza katika kuimarisha uchumi wa nchi.

Mfanyabishara Frola Ayo, ameomba zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi liwe endelevu kwani linajenga urafiki baina yao na TRA na hivyo litaongeza uhiari wa kulipa kodi kwa wakati.

"Kutokana na elimu hii hakika tutalipa kodi ipasavyo kwa sababu inatuweka karibu na TRA suala ambalo linatuondolea hofu na pia tunaomba elimu hii iwe endelevu ili wafanyabiashara wengi waweze kujijenga zaidi na kuimarika katika biashara zao,”

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani Mwanza inafanyika pia katika Mkoa wa Morogoro na Mbeya na imelenga kuwaelimisha walipakodi juu ya mambo mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja na kupokea maoni, kusikiliza kero na changamoto za walipakodi hao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live