Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mongella afafanua kusitisha uokoaji usiku

18632 Pic+mongela TanzaniaWeb

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukerewe. Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella ametoa ufafanuzi kuhusu zoezi la uokoaji kusitishwa juzi usiku Septemba 20, 2018 akisema ulitokana na ushauri wa wataalam wa uokoaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 22, 2018 katika mwalo la Kisiwa cha Ukara anakoongoza zoezi la uokoaji, Mongella amesema wazamiaji walishauri uokoaji usitishwe hadi jana asubuhi kutokana hali mbaya iliyoanza kujitokeza chini ya maji nyakati za usiku.

"Zoezi hili linafanyika kitaalam na wazamiaji wabobevu wanaofanya kazi kwa saa 24 ambao ilipofika usiku walishauri watu wasizame tena chini ya maji. Mimi kama msimamizi nisiye na utaalam wa kuzama majini sikuwa na namna nyingine zaidi ya kuwasikiliza," amesema Mongella

"Nisingetumia kofia yangu ya ukuu wa Mkoa na msimamizi wa zoezi la uokoaji kulazimisha waendelee kuzama kwa sababu uamuzi huo ungeweza kusababisha madhara zaidi ikiwemo kuwapoteza wataalam na kuongeza matatizo zaidi."

Amewasihi Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kuzungumzia kwa busara na staha ajali hiyo kuepuka kuongeza machungu kwa waliopoteza ndugu na kujeruhiwa katika ajali hiyo.

Ufafanuzi huu wa Mongella umekuja katikati ya mjadala miongoni mwa Watanzania kuhusu taarifa za uokoaji kusitishwa usiku wa Septemba 20 kutokana na giza.

Mv Nyerere inayofanya safari kutoka Bugolora kwenda kisiwa cha Ukara kimezama Septemba 20 ambapo hadi sasa maiti zaidi ya 151 zimeopolewa  huku watu 40 wakiokolewa wakiwa hai.

Kivuko hicho kina uwezo wa kupakia abiria 101 na tani 25 ya mizigo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz