Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mongela asisitiza chanjo wahudumu sekta ya utalii

A26f406d5786efaf9fac36e5d7b2f18a Utalii Arusha

Tue, 10 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amewataka wanaofanya shughuli za utalii kuchanjwa ili watalii kutoka nje ya nchi wawe na amani.

Mongella alisema hayo juzi alipokuwa akikagua zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 katika ofisi za chama Cha Waongoza Utalii Tanzania (TATO),Jijini Arusha.

Alisema mtalii anapokuja Tanzania atapenda kuhudumiwa na watu waliochanjwa kuanzia dereva hadi muongoza watalii, hivyo ni vizuri wadau wa sekta hii kuichukulia chanjo hii kama ni njia ya kurudisha hali nzuri ya utalii mkoani hapa.

Aliwataka wakurugenzi wa makampuni ya utalii kuwahamasisha wafanyakazi wao kupata chanjo ili iwe rahisi kwao kupata kazi nyingi kutoka kwa watalii hao.

Aidha, alipongeza uongozi wa Chama Cha Waendesha Watalii Tanzania (TATO) kwa kuwahimiza wanachama wao kupata chanjo ya UVIKO 19, na kusisitiza serikali kuendelea kushirikiana nao kwa kuhakikisha hali ya utalii inarudi kama awali.

Naye, Mwenyekiti wa TATO ,Wilbad Chambulo alisema wao kama wadau wa utalii wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuchanjwa kwani hakuna mtalii kutoka nje atakaependa kufanya kazi na mtanzania ambae hajachanjwa.

Aliwasisitiza wanachama wa chama hicho hasa waliochanjwa kuwahamasisha wenzao ambao hawajachanjwa waweze kupata chanjo hiyo mapema kwani hali ya utalii katika Mkoa wa Arusha imeanza kuimarika kidogo.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Serengeti Balloon Safari, John Course aliipongeza serikali kwa kukubali watanzania wachanjwe chanjo ya UVIKO 19.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dk Silvia Mamkwe alihimiza wananchi kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19 kwani ili nchi iweze kuwa huru na janga hili inahitaji kuwa na watu waliochanjwa kati ya asilimia 60 hadi 80.

Chanzo: www.habarileo.co.tz