Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mnyeti ampa siku saba DED Kamoga kuhamia Dongobesh

82084 Mnyeti+pic RC Mnyeti ampa siku saba DED Kamoga kuhamia Dongobesh

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbulu. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amempa siku saba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga, kuhamia katika Kata ya Dongobesh kwenye makao makuu mapya ya halmashauri hiyo.

Hata hivyo, Kamoga amesema walishaanza mchakato wa kuhamia kwenye kata hiyo ili kusogeza huduma karibu na jamii.

Mnyeti ametoa agizo hilo leo Oktoba 28, 2019 wakati akikagua ujenzi wa majengo ya makao makuu mapya ya halmashauri ya wilaya ya Mbulu yanayojengwa kwenye Kata ya Dongobesh.

Amesema agizo la Rais John Magufuli alilolitoa la kila halmashauri ihamie kwenye eneo lake linapaswa kufanyiwa kazi kwa kutekeleza na kuhama mara moja.

“Nilikuwa nakupa siku saba pekee za kuhama ila kwa sababu umesema umeanza utekelezaji basi nakutakia kila la heri muhamie Dongobesh,” amesema Mnyeti.

Pia, amewataka wananchi wa Kata ya Dongobesh kuwapa ushirikiano watumishi wa halmashauri hiyo wanaohamia kwenye eneo hilo.

Amesema endapo wananchi hao hawatawapokea vizuri watumishi, halitakuwa jambo zuri kwa sababu lengo lao ni kutumikia ipasavyo jamii ya eneo hilo.

“Muwapende watumishi na kuna wanaume wengine hawajaoa muwape wachumba na wasichana ambao hawajaolewa vijana changamkieni fursa ili watumishi wasihame,” amesema Mnyeti.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga amesema wameanza kuhamisha baadhi ya vitendea kazi vilivyopo Mbulu mjini.

“Tutahakikisha hata kikao kijacho cha baraza la madiwani kitafanyika hapa Dongobesh ili kuzoea mazingira ya makao makuu mapya ya halmashauri yetu,” amesema Kamoga.

Kwenye mkoa wa Manyara kuna halmashauri mbili za wilaya ya Babati na wilaya ya Mbulu ambazo hazikuwa zinafanya kazi kwenye maeneo yao zaidi ya kufanyia mjini Babati na Mbulu mjini.

Chanzo: mwananchi.co.tz