Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC: Mkipiga kura rudini nyumbani

D97c39a65a23be10094011b3aebb3f57 RC: Mkipiga kura rudini nyumbani

Sun, 25 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack amewataka wananchi wenye sifa, wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu na wakishapiga warudi nyumbani kusubiri matokeo.

Amesisitiza kuwa siku hiyo ya kupiga kura, amani na utulivu vitatawala vituoni, hivyo wasiwe na hofu yoyote.

Telack alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya upigaji kura.

Aliwaeleza waandishi kuwa wasijaribu kutangaza matokeo siku hiyo, kwani wapo wahusika wenye kufanya kazi hiyo ya kutangaza.

Alisema wale wanaojiandaa kufanya vurugu hatua kali ya kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Ulinzi utakuwepo wa kutosha. Vituo vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi jioni. Pia siku hiyo shughuli za kijamii zitaendelea kama kawaida na asiwepo mtu wa kuzuia kwani serikali imejipanga,”alisema.

Telack alisema kuwa matokeo siku hiyo yatatangazwa kwa mujibu wa sheria na hakuna mtu wa kuiba kura.

Alisema wapo mawakala wa kila chama walioaminiwa. Alisema uchaguzi ni mchakato, ulianza mapema na utapita na maisha yataendelea.

"Uchaguzi ni sawa na mchezo wa mpira, lazima mshindi apatikamne. Kuna kufungwa na kufunga, hivyo wanaoshindana lazima wakubaliane na matokeo ili maisha ya kila siku yaendelee. Ninyi waandishi msitangaze matokeo kwa mihemko. Wapo wenye jukumu la kutangaza,”alisema Telack.

Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga alisema wameshapokea tayari vifaa vya uchaguzi. Alisema vipo vituo vya kupigia kura 2,700 na kila kituo kina mtendaji mkuu, wasaidizi wanne na mlinzi mmoja.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi alisema wameshaapisha mawakala 326 kutoka vyama vilivyosimamisha wagombea. Aliwataka watumie viapo hivyo, kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinakuwepo siku ya uchaguzi.

Chanzo: habarileo.co.tz