MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amemsimamisha kazi mwezi mmoja Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Zacharia Awe, kwa madai ya kukwamisha kasi ujenzi vyumba vya madarasa.
Mjema amemsimamisha kazi Afisa huyo leo, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu.
Alisema, amefika wilayani humo kukagua utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa, na kukuta eneo la ujenzi hakuna vifaa vya ujenzi, na alipohoji aliambiwa mpaka Afisa manunuzi aamuue ndipo vinunuliwe.
"Katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mmeniangusha sana kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa, nimefika site hakuna hata nondo eti mpaka Afisa Manunuzi aamue," alisema Mjema.
"Hivyo kuanzia sasa Afisa manunuzi na kusimamisha kazi hadi Decemba, Mkurugenzi naomba nitafutie mtu mwingine ambaye ataendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassani, ili tukamilishe madarasa haya 81 wilayani Kishapu," aliongeza.
Aidha, alitoa maagizo pia kwa Mkuu wa Usalama wilaya, Mkuu wa wilaya, pamoja na Mkurugenzi, kuwasimamia utendaji kazi, Afisa Mipango, Ardhi, pamoja na fedha, ili kufanikisha ujenzi huo wa vyumba vya madarasa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, aliwataka watumishi wa Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Kishapu, wabadilike kiutendaji kazi, kuwa na mshikamano, uwajibikaji, pamoja na kutunza siri za Serikali ili kusukuma gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, alimwahidi Mkuu huyo wa Mkoa, kuwa maelekezo yote ambayo ameyatoa atayafanyia kazi, ili kuhakikisha Kishapu inasongambele kimaendeleo.