Moshi. Waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania leo Jumanne Julai 30, 2019 wameondolewa katika ukumbi mdogo wa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kwa madai hawaruhusiwi kuwepo kwenye kikao cha wafanyabiashara kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Anna Mghwira.
Kikao hicho cha wafanyabiashara wa Hai kimehudhuriwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, ikiwa ni siku chache baada ya mfanyabiashara na mmiliki wa Hoteli ya kitalii Weruweru, Cathbert Swai kumtuhumu Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kumnyanyasa na kumwomba rushwa.
Mfanyabiashara huyo alitoa malalamiko hayo Julai 22, 2019 kwenye kikao kilichoitishwa na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Msafiri Mbibo kwa ajili ya kujadili na kuzifanyia ufumbuzi changamoto zinazowakabili katika ulipaji wa kodi.
Hata hivyo, leo Julai 30, 2019 wakati RC Mghwira alipoingia kwenye kikao hicho, aliwataka waandishi wote kutoka ndani ya ukumbi huo na kwamba baada ya mazungumzo na wafanyabiashara hao atazungumza na vyombo vyote vya Habari.
"Naomba waandishi wote mtoke nje ya huu ukumbi, tukimaliza tutawaita tuzungumze na nyie," amesema RC Mghwira