Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mghwira awaonya watendaji wanaowabughudhi wafanyabiashara

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema watumishi watakaofanya vitisho kwa wafanyabiashara waliowekeza katika mji wa Moshi watachukuliwa hatua kali kama wahalifu wengine.

Mghwira ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 23, 2019 mara baada ya kukutana na wafanyabiashara hao pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali ili kujua changamoto zinazowakabili.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kutokana na mgogoro unaoendelea katika jengo la Stendi ya Moshi baina ya manispaa  na wawekezaji waliowekeza katika jengo hilo kwa miaka mingi, ameiagiza halmashauri hiyo kukaa meza moja na wafanyabiashara hao ili kutatua mgogoro wa viwango vipya vya kodi.

Amesema haridhishwi na uamuzi wa halmashauri hiyo kupandisha kodi ya vibanda kutoka Sh30,000 kwa mwezi hadi Sh400,000, baada ya mkataba wa uwekezaji kumalizika Desemba 31, 2018.

Mghwira amesema tozo hiyo ya kodi ya vibanda iliyofanywa na manispaa hiyo ni kuwaumiza wafanyabiashara hao na kutotambua umuhimu wao katika ujenzi wa vibanda hivyo ambavyo waliwekeza katika jengo hilo na kuchangia ujenzi Sh4.5milioni.

Amesema hatokubali Serikali ipakwe tope kutokana na uamuzi huo wa manispaa na kusema kufanya hivyo ni kuonyesha dhahiri Serikali imeshindwa kuwatambua na kuthamini mchango wa wafanyabiashara hao.

"Hii kodi mliyoiweka si sahihi kaeni na hawa wafanyabiashara kwa sababu mnachokifanya mnataka kusema Serikali imeshindwa na kutothamini michango ya wafanyabiashara hawa waliotoa miaka 15 iliyopita kwa kuchangia ujenzi wa jengo," amesema.

"Sitakubali Serikali ipakwe matope na uamuzi wenu mmeenda mbali mno kutoza kodi kubwa kiasi hiki, mtu aliyechangia ujenzi ni tofauti na mtu anayekuja na kuwa na dau kubwa ambaye hajachangia ujenzi wowote, kaeni mezani mlete takwimu zinazoeleweka" amesema Mghwira.

"Manispaa narudia tena kaeni na wafanyabiashara hawa, fuateni vigezo na viwango vilivyopo sokoni, soko hili ni huria si soko holela, wekeni bei ambayo haiwaumizi wafanyabiashara hawa kwa sababu wana mchango mkubwa katika ujenzi wa jengo hili," amesema Mghwira.



Chanzo: mwananchi.co.tz