Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mghwira atoa sababu za kuibuka kipindupindu

18002 Pic+rc TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ametaja chanzo cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika vijiji vilivyopo jirani na mkoa wa Manyara ni matumizi ya maji yasiyosafi na salama kutoka bonde la mto pangani.

Akiozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 18,2018 baada ya habari za mlipuko wa kipindupindu katika mkoa huu kusambaa kwa kasi.

Ametaja sababu nyingine ni kukosekana kwa vyoo kwenye baadhi ya wakulima wa mashamba makubwa ya umwagiliaji katika bonde hilo la mto pangani ambako watu wanafanya shughuli za kilimo.

Hata hivyo, amesema ukosefu wa vyoo hivyo uliosababishwa na mvua kubwa zilizopita katika kipindi cha masika zilisababisha vyoo kuharibika.

“Maji ya Bonde la Mto Pangani hufanyiwa uharibifu na wananchi wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa juu, hivyo wananchi wa ukanda wa chini ambao hutumia maji hayo kwa matumizi yao wapo hatarini kupata ugonjwa huo,” amesema Mghwira.

Mghwira amesema hadi juzi wagonjwa waliopatikana kuwa na ugonjwa huo ni 26 ambao wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya TPC na wagonjwa watano wanatoka maeneo ya Kirungu, Newland, Chemchem Wilaya ya Moshi na hao wengine 21 wanatoka eneo la Msitu wa Tembo huko Manyara.

 “Ugonjwa huu umeenea kutokana na  mwingiliano na wananchi wa msitu wa Tembo huko Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara; mgonjwa mmoja mwanaume aligundulika na vimelea vya kipindupindu baada ya kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Mawenzi,” amesema Mghwira.

Amesema tahadhari za kuwatenga wagonjwa hao ili ugonjwa usiendelee kuenea, zimeendelea kuchukuliwa huku wakiendelea kupata matibabu, pamoja na kutoa elimu kwa kaya ili wananchi waweze kupata uelewa namna ugonjwa huo unavyoenea.

Hata hivyo, Mghwira ameagiza viongozi wa maeneo hayo kusimamisha shughuli za kilimo  hadi wakulima  watakapojenga vyoo pamoja na wananchi wenyewe kuchukua tahadhari za haraka kwa kuwa ugonjwa huo husambaa kwa kasi.

Chanzo: mwananchi.co.tz