Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mbeya avua kofia moja Iringa

13946 RC+PIC TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema imemlazimu kuachia nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa kwani ameambiwa achague kitu kimoja kati ya nafasi hizo mbili.

Chalamila aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Julai 28, wakati huo akiwa tayari na cheo cha mwenyekiti wa CCM Iringa.

Akizungumza na viongozi wa dini mkoani humo Agosti 9, Chalamila alisema ingawa baadhi ya wana CCM wanamlazimisha kuachia cheo kimoja, asingeachia uenyekiti wa CCM.

Lakini, jana Chalamila akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Sido jijini Mbeya akiwa ameambatana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliofika hapo kwa lengo la kutoa elimu ya kulipa kwa wafanyabiashara wa soko hilo alisema anaachia uenyekiti wa CCM.

Chalamila alilazimika kuweka bayana hayo baada ya mfanyabiashara katika soko hilo, Mohamed Miraji kumueleza kwamba kauli za viongozi wa kisiasa zinachangia kurudisha nyuma juhudi za wananchi katika maendeleo kutokana na tofauti za itikadi za kisiasa.

“Lakini kuna kauli za wanasiasa zinatuvunja moyo. Mwanasiasa anasema uamuzi wa kuleta maendeleo sehemu fulani unaletwa na CCM, lakini kuna wengine wanachangia kodi hawana vyama na wengine ni wafanyakazi watumishi wa umma wanachangia kodi,” alisema.

Alisema jambo hilo linawaumiza wananchi kwa sababu ili wananchi walipe kodi ni lazima washikamane na kujiletea maendeleo.

“Hivyo mkuu wa mkoa wetu (Mbeya) tusingependa kusikia kauli kama hizo,” alisema Miraji.

Akijibu hoja za Miraji, RC Chalamila alisema, “Mimi kweli ni mwanasiasa, ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, lakini Mbeya ni Mkuu wa Mkoa, ila kule (Iringa) lazima nitaachia tu hakuna namna, kwa sababu nimeambiwa nichague kitu kimoja. Sasa na wao wananiambia nichague kitu kimoja huku ukuu wa mkoa na uenyekiti wa chama wanategemea nitaenda wapi?” alisema Chalamila

Alisema kuna wakati kwa sababu labda Mbeya ni ya Chadema, au kwa sababu kata fulani ni ya CCM maendeleo hayafiki kwa sababu ni upinzani.

“Sisi wanasiasa tuna vikauli vinavyochukiza lakini mvione kama ni vikauli vya Yanga na Simba, vikauli vya Manchester United na Real Madrid, vikauli vya Wasafwa na Wanyakyusa au mvione kama vikauli vya Wahehe na Wabena, lakini tusihamishie mihemko hiyo kwenye maendeleo,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz