Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mbeya atoa siku saba machinga kuondoka maeneo wasiyotakiwa

29757 RCMBEYA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ametoa siku saba kwa wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) wanaofanyia biashara zao nje ya soko Kuu la Mwanjelwa na stendi ya daladala ya Kabwe na katika hifadhi za barabara katikakati ya jiji la Mbeya kuvunja vibanda vyao na kuondoka kwa hiari.

Chalamila  ametoa msimamo na amri hiyo leo Jumamosi Desemba 1, 2018 alipozungumza na wafanyabiashara wa Mwanjelwa, Kabwe na Sido jijini hapa ambapo amesema waliwekwa katika maeneo hayo kwa muda wakati uongozi wa Jiji la Mbeya ukiwatafutia maeneo salama ya biashara zao na sasa yamepatikana.

Amesema licha ya wafanyabiashara hao kuwekwa kwa muda katika maeneo hayo mwaka 2016, lakini baada ya kukamilisha miundombinu yote ya maeneo walikopanga kuwapeleka mwaka huohuo machinga hao waligoma jambo ambalo amesema ifikapo Ijumaa wiki ijayo wawe wameondoka wenyewe vinginevyo atatumia nguvu.

“Haiwezekani soko hili (Mwanjelwa) nzuri na la kimataifa halafu likazungukwa na vibanda vya mbao nje na nyinyi (wamachinga) mkalipa kodi ya Sh40,000 wakati maduka ya ndani yakiwa tupu kwa madai bei ya kodi ni kubwa,” amesema Chalamila

“Hivyo basi natangaza rasmi gharama ya vyumba, maduka ya chini kila chumba kitakodishwa kwa Sh150,000, badala ya Sh200,000 na maduka ya katikati vyumba vya kawaida itakuwa Sh50,000 na vyumba vikubwa, mfanyabiashara atakayewahi atafanya mazungumzo na uongozi wa Jiji.”

“Lakini kule juu (ghrofa ya tatu) bei ya chumba itakuwa Sh30,000. Hivyo nyinyi mlioweka vibanda vya mba, mkataba wenu umekwesha jana Ijumaa na ifikapo Ijumaa wiki ijayo muwe mmebomoa wenyewe hivyo vibanda na anayetaka kufanya biashara aingie ndani ya Soko hili,” amesema Chalamila.

Pia Chalamila amesema wafanyabiashara hao na wanaofanyia biashara zao stendi ya daladala ya Kabwe wanatakiwa kuondoka na kwenda kwenye masoko ya Sido, Mwanjelwa au nane nane ifikapo Ijumaa wiki ijayo kwa hiari yao kabla ya kushurutishwa kama watakutwa maeneo hayo.

“Sitaki kusikia sauti ya tofauti hapa, nimeshasema na sijaribiwi katika hili, haiwezekani wengine tukawalipisha kodi halafu nyinyi mkaendelea kufanya biashara zao maeneo yasiyoruhusiwa, kule nane nane Jiji lilishawatengenezea miundombinu yote muhimu na kuna maduka 1,102 lakini hadi walioingia ni wamachinga 28 tu, wengine hamtaki, sasa nasema hapa mliwekwa kwa muda tu,” amesema

Chalamila ameuagiza uongozi wa Jiji la Mbeya atakayekaidi kutekeleza hilo basi akamatwe na kuswekwa rumande kimyakimya na kisha afunguliwe mashtaka ya kutotii amri halali ya Serikali kwani atakuwa ana mpango wa kuendelea kuhujumu mapato ya Serikali na kuhatarisha amani ya Mbeya.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mbeya, James Kasusura  amemueleza Chalamila Jiji la Mbeya limeendelea kukosa mapato yake kutokana na wafanyabiashara hao kugoma kwenda maeneo yaliyotengwa kwa biashara huku miundombinu yote ikiwa sawa.

“Katika hili tunaona njia pekee ya masoko haya kupata watu ni kuona wafanyabiashara walioko nje ya soko la Mwanjelwa kuondoka na kuingia ndani ya soko, lakini walioko stendi ya Kabwe kuondoka na kwenda nane nane,” amesema

Wakati huo huo, Chalamila ametangaza safu mpya ya viongozi wa Sido baada ya uongozi wa awali kuuvunja kwa madai walikuwa chanzo cha migogoro baina ya wafanyabiashara na uongozi wa Jiji, pia kuwatapeli wafanyabiashara wenzao.

Wakati Chalamila akitoa tamko hilo, baadhi ya wafanyabiashara walianza kulia huku wengine wakifurahia hususani wale wanaofanyia biashara zao ndani ya soko la Mwanjelwa.

Mmoja wa wafanyabiashara wa Mwanjelwa, Subira Mwakifwamba amesema, “Unajua mimi nauza matunda yangu kwenye kizimba hiki ndani ya soko na nalipa ushuru wa Sh5,00 kila siku lakini mwenzangu mwenye matunda kama yangu anafanyia nje na hataki kuja huku unafikiri mteja atakuwa na muda kuingia ndani?.

“Haya kuna mwingi ana duka ndani  na analipa kodi ya pango Sh200,000 lakini yupo mwingine nje kaweka banda ya mbao na anauza bidhaa ile ile lakini analipa kodi ya Sh40,000 je hapo unafikiri kuna mtu atakubali kuingia ndani ya soko? Lakini kwa amri hii sasa biashara itafanyika tu wote tuingie ndani na kama kuumia basi tuumie sote,” amesema



Chanzo: mwananchi.co.tz