Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameagiza wakuu wa Wilaya, waratibu elimu kata kufanya msako nyumba kwa nyumba kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza wataoshindwa kuripoti shule.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Januari Mosi 2023, amesema jumla ya wanafunzi 45,595 wanatarajia kuanza masomo Januari 9, 2023.
”Kwa mkoa hakuna uhaba wa vyumba vya madarasa kwani tumefanikiwa kujenga vyumba 1,000 ambavyo vimejitoshereza na kuwepo kwa ziada kwa kutumia mapato ya ndani kwa kila halmashauri, sasa isitokee mtoto akabaki nyumbani,” amesema.
Amesema kama mkoa hawako tayari kuona mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza akabaki nyumbani, ni lazima ufanyike msako wa nyumba kwa nyumba ikiwa ni pamoja na wazazi kuchukuliwa hatua.
“Wakuu wa wilaya, waratibu elimu kama nimewapa jukumu hilo ni lazima lifuatiliwe ikiwa ni pamoja na maeneo yenye jamii ya wakulima na wafugaji hakikisheni kila mtoto aliyechaguliwa anaripoti shuleni,” amesema.
Wakati huo huo Homera ameagiza wakuu wa wilaya kuondoa makundi ya mifugo ambayo inaingizwa katika maeneo yasiyo rasmi na kuona namna ya kutenga maeneo kwa mifugo.
“Kumekuwepo na changamoto kubwa wafugaji mifugo inaondolewa wanarejesha tena sasa sitopenda kuona mifugo ikifugwa kiholela bali Madc angalieni katika maeneo yenu,” amesema
Mkazi wa Jijini hapa, Christian Joel ameiomba Serikali kuthibiti ajira za utotoni kwani kuna changamoto kubwa kwa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba wazazi kuwapeleka kufanya kazi mikoani.
“Hilo ni tatizo kubwa sana kwa Mkoa wa Mbeya mzazi mtoto akimaliza darasa la saba aoni kama kuja umuhimu wa kupata elimu ya sekondari na badala yake kutanguliza maslai mbele kwa kuwatumikisha ajira za utotoni ambazo zinazima ndoto zao,” amesema.