Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mbeya aagiza kukamatwa katibu wa CCM aliyetokomea na Sh20,000 za rambirambi

22589 Ccm+pic TanzaniaWeb

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ameagiza Katibu wa CCM kata ya Maanga jijini Mbeya,  Norasco Tibakawa  kukamatwa na kuwekwa rumande saa 24 baada ya kudaiwa kutafuna Sh20, 000 za rambirambi.

Chalamila ametoa amri  hiyo leo Jumanne Oktoba 16, 2018 wakati akisikiliza kero za wananchi wa kata  hiyo.

Mkazi wa kata hiyo, Flora Mwakipesile amesema kuwa katibu huyo hajamkabidhi fedha za rambirambi tangu alipofiwa na mdogo wake Novemba, 2018.

Flora amesema wanachama wa CCM kata hiyo wana utaratibu wa kuchangiana fedha lakini alipopatwa na msiba hakukabidhiwa rambirambi hizo  licha ya wanachama kuchanga.

Amesema katibu huyo ndio alipewa jukumu la kukusanya fedha kwa wakati huo.

Flora amefafanua kwamba amekuwa akifuatilia fedha hizo kwa zaidi ya miezi 11 bila mafanikio, kuna wakati alielezwa  fedha zilikuwa tayari na kila alipomfuata katibu huyo alimpiga chenga.

“Nilifiwa na  dada yangu na huwa tuna utaratibu wa  kuchangiana fedha mtu anapokumbwa na matatizo. Tumefanya hivyo kwa watu wengi lakini ilipofika zamu yangu watu walinichangia cha kushangaza hadi sasa sijapewa fedha hizo,” amesema Flora.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo,  Chalamila akamtaka katibu huyo kutoa majibu ambapo alikiri kwamba hadi sasa hajamkabidhi fedha hizo kwa kuwa mlalamikaji amekuwa hapatikani kila anapokwenda nyumbani kwake.

“Mkuu wa Mkoa ni kweli fedha hizi hatujamkabidhi kwa sababu mchango ulisuasua hadi msiba unaisha tulikuwa bado tunachangisha, lakini hata hivyo mchangishaji alipatwa na tatizo alizitumia na baadaye akazirejesha kwangu,” amesema Tibakawa.

Kutokana na maelezo hayo, Chalamila akaamuru katibu huyo kuwekewa rumande saa  24, na kubainisha kuwa ana nia ya kukihafua CCM.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Wilson Nkhambako amesema chama hicho hakiwezi kumvumilia mtu yoyote ambaye ana nia ovu ya kukichafua chama hicho.

Amesema katibu huyo ataitwa katika kikao cha kamati ya maadili ajili ya  kuhojiwa na kuchunguzwa tuhuma zinazomkabili.

Chanzo: mwananchi.co.tz