Mkuu wa mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee ameagiza kukamatwa kwa meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Serengeti, Michael Alphonce kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ujenzi wa barabara ipasavyo.
Pia ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa haraka kuhusu mradi huo ili kuweza kubaini kama utejelezaji wake umezingatia mkataba ili hatua ziweze kuchukuliwa endapo itabainika kuwa utekelezaji wake umekwenda kinyume.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa maagizo hayo jana Jumatano Februari 22, 2023 baada ya kufanya ziara na kukagua mradi huo wa ujenzi wa barabara hiyo iliyopo mjini Mugumu na kubaini mapungufu kadhaa ikiwemo mitaro iliyojengwa chini ya kiwango.
"Serikali inatoa fedha nyingi kwaajili ya miradi ya maendeleo lakini wasimamizi wamekuwa hawatekelezi wajibu wao miradi inajengwa chini ya kiwango wizi wa vifaa unafanyika hakuna hatua zinazochukuliwa," amesema.
Barabara hiyo ya mjini Mugumu yenye urefu wa kilomita 1.45 inatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh923 milioni na hadi sasa imefikia asilimia 95 za utekelezaji wake.
Akizungumzia agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vicent Mashinji amesema kuwa agizo hilo litatakelezwa ndani ya siku 14 kuanzia sasa na hatimaye hatua za kinidhamu na kiutumishi kuchukuliwa baada ya uchunguzi.
"Bahati nzuri hata sisi ngazi ya wilaya tulishabaini mapungufu kadhaa kwenye mradi na tumeagiza Takukuru wafanye uchunguzi ili kubaini mapungufu kwa kitaalamu zaidi na hatua za kinidhamu na kiutumishi zichukuliwe kwa kila atakayebainika," amesema
Kwa upande wake Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia miradi wanashindwa kutekeleza wajibu wao kama ipasavyo.
"Pesa zinaletwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi lakini inasikitisha kuona kuwa wenye dhamana ya kusimamia wanashindwa kutekeleza wajibu wao.
“Nimshukuru mkuu wa mkoa kufika hapa na kutoa maagizo naamini hatua zitachukuliwa," amesema.