Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Malima azungumzia ujenzi Uwanja wa Ndege Musoma

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ameiomba Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuharakisha ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma ili kuchochea maendeleo mkoani humo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 24, 2018 mbele ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Elias Kwandikwa aliyepo mkoani Mara kwa ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo.

Malima amesema uwanja huo ukijengwa na kukamilika utakuwa kichocheo kikuu cha maendeleo na uchumi kutokana na umuhimu wake katika sekta ya utalii na usafirishaji.

Amesema Mkoa wa Mara unakosa mapato ambayo yangepatikana endapo uwanja huo ungekuwa unafanya kazi kama inavyotakiwa.

Ametolea mfano wa uwanja mdogo wa ndege wa Soronera uliopo ndani ya hifadhi ya Serengeti, akibainisha kuwa Serikali hukusanya zaidi ya Sh300 milioni kwa mwezi kutokana na ndege zinazotua uwanjani hapo zikiwa na watalii.

Amesema tayari uongozi wa mkoa umefanya m,aandalizi kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo ikiwa ni pamoja na tathmini ya fidia kwa wakazi wa maeneo ya uwanja huo.

Amesema zaidi ya nyumba 100 zinatakiwa kubomolewa huku zikitengwa zaidi ya Sh4.5 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia.

Kwa upande wake Kwandikwa ameahidi kushughulikia maombi hayo ili uwanja huo uweze kujengwa kwa haraka.



Chanzo: mwananchi.co.tz