MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amesema wanunuzi binafsi wataruhusiwa kununua kahawa kupitia vyama vya ushirika badala ya kwenda moja kwa moja kwa wakulima.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli wakati akizungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamisheye, Kemondo Muleba, Nyakabango na Kyamyorwa mkoani Kagera Julai mwaka jana.
Akizungumza jana wakati wa kikao kazi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa, Profesa Jamali Adam, alisema Serikali iliamua kuanzisha ushirika ili wakulima wauze mazao yao kwa bei nzuri, hivyo wanunuzi binafsi wanapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Uuzaji mazao ya wakulima kupitia vyama vya ushirika tumeuweka ili wakulima wakiibiwa au kupunjwa iwe rahisi kumpata muhusika na tunachukua hatua kali dhidi ya wote watakaofanya ubadhirifu, lakini tukimkuta mnunuzi binafsi ameingia mpaka shambani ni kama ameingia chumbani, atapata balaa,” alisema Malima.
Aliitaka Bodi ya Kahawa kutafuta wanunuzi binafsi kadiri iwezavyo ili kuongeza ushindani na wakulima waweze kupata bei nzuri kwani jambo hilo litasaidia kukabiliana na unyonyaji dhidi ya wakulima wa kahawa pamoja na mazao mengine mkoani Mara.
“Mkulima yeyote akisikia bei nzuri ya kahawa lazima atauza, hawezi kwenda kwenye bei ndogo wakati ameona kuna mahala kuna bei nzuri inayoendana na jasho lake,” alisema Malima.
Pia aliipongeza Bodi ya Kahawa kwa kutoa miche 40,000 kwa Mkoa wa Mara na kuishauri kuwaongezea wakulima miche mingi zaidi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa, Profesa Adam alisema wamejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji kuhakikisha kunakuwa na bei nzuri na kujenga mazingira bora ya biashara kwenye tasnia ya kahawa.
Alisema bodi itaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo ya Serikali ikiwemo upatikanaji wa miche bora kwa wakulima, malighafi kwenye viwanda vya kahawa na kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri na kuongeza ushindani kwenye soko la kahawa la awali na soko la pili.
Aidha aliwataka wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini walioombwa vibali na wanunuzi binafsi na wenye viwanda kufanya hivyo kwa wakati ili bodi iweze kutoa leseni mapema.