Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Malima alia na wanaoharibu vyanzo vya maji Tanga

Malima Tanga Maji Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Tanga

Thu, 31 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amezitaka jumuiya za watumiaji wa maji kudhibiti uharibifu wa mazingira ili kulinda vyanzo vya maji.

Ameyasema hayo Machi 30 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa pili wa jukwaa la wadau wa usimamizi wa rasilimali za Bonde la Mto Pangani uliofanyika mjini Tanga.

RC Malima pia amebainisha kuwepo kwa waharibifu wa mazingira katika baadhi ya vyanzo vya maji na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua.

"Kuna mtu nimembaini maeneo ya Halmashauri ya Bumbuli kuwa anafanya uchafuzi mkubwa wa mazingira kwa kuchimbaji madini kwenye vyanzo vya maji," amebainisha Malima bila kumtaja mtu huyo na kuagiza achukuliwe hatua za kisheria.

RC Malima amesema Wilaya ya Lushoto ilikuwa kijani na ilikuwa mtu akisimama maeneo ya chini alikuwa anaona milima inavyotiririsha maji kama ilivyo kwa milima ya Uluguru ya Morogoro.

“Lakini nenda kaangalie sasa hivi. Hakuna maji yanayotitirika kutoka milimani. Hii inatokana na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji na misitu unaofanywa na wananchi kwa ajili ya kukata miiti au kuchimba madini," amesema Malima.

Akijibu maagizo ya RC Malima, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalisti Lazaro amesema washaanza kuyafanyia kazi.

"Mkuu maagizo yako tumeshayatekeleza ikiwemo kuwafikisha Polisi watu watatu waliokuwa wanachimba Madini katika eneo hilo."

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Bonde la Mto Pangani, Segule Segule ameonya kama shughuli za kibinadamu hazitadhibitiwa katika bonde hilo, huenda zikasababisha upungufu wa maji kwa wananchi wapatao milioni 5.6 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Tanga wanaotegemea bonde hilo.

Segule amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji hususani maeneo ya Lushoto, Muheza katika upande wa msitu wa Amani pamoja na changamoto ya ukataji wa miti katika maeneo ya hifadhi na vyanzo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live