Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa onyo kwa mtu atakayenunua makontena yake 20 yaliyo bandarini kuwa atalaaniwa yeye na uzao wake.
Juzi, makontena 20 yenye samani za ndani kama vile meza, viti na mbao za kufundishia yalikosa wanunuzi katika mnada kutokana na watu wengi kushindwa kufikia bei iliyotajwa.
Makontena hayo na mali nyingine yanapigwa mnada kutokana na kushindwa kulipiwa kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Makonda alisema jana alishiriki ibada mjini Ngara mkoani Kagera kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa anaamini Mungu alimpa kwa ajili ya walimu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Mwananchi ilimpigia simu Makonda jana baada ya kuthibitisha kuwa ni makontena yake ili kujua jitihada anazochukua kuhakikisha hayauzwi na badala yake yanatolewa kwa walimu kama yalivyokusudiwa.
“Leo (jana) nimekwenda katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Anglikana mjini Ngara, nimefanya ibada maalumu kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa mkoa wangu,” alisema Makonda.
Alisema kupatikana kwa samani hizo ni jitihada zake binafsi za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi walimu ikiwa ni kumuunga mkono Rais John Magufuli aliyeamua kutoa elimu bure kwa Watanzania na hasa watoto wa masikini.
“Rais alitambua umuhimu wa elimu ndiyo maana kama msaidizi wake sikuona sababu ya kukaa kimya wakati mazingira ya walimu si rafiki na kusubiri kuwalaumu pale watoto wanapofeli bila kufanyia kazi changamoto zao,” alisema Makonda ambaye kabla ya kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alikuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni.
“Baada ya kuona jitihada za Rais katika sekta ya elimu, kwa kutoa elimu bure nami nikawaza kama msaidizi wake, nafanya nini kuunga mkono kazi nzuri anayoifanya Rais.”
“Ndipo Mungu aliweka wazo lake ndani ya moyo wangu juu ya ujenzi wa ofisi za walimu kama sehemu ya kuboresha mazingira yao. Kwa utukufu wake Mungu, akaandaa watu wa kuchangia tena kutoka nje na ndani ya nchi,” alisema Makonda.
Akitumia maneno ya vitabu vitakatifu, Makonda alisema utukufu wa Mungu umejidhihirisha kwa Watanzania kuchangia, wakiwemo askari wa Jeshi la Kujenga Taifa waliojitolea kujenga majengo; benki kwa kununua saruji; baadhi ya viwanda kutoa mabati na nondo na wengine kujitolea masinki, mabomba na taa.
Makonda alisema nchi ya China imejenga ofisi, huku Watanzania wanaoishi Marekani wakimpatia samani za walimu ambazo zipo kwenye makontena zaidi ya 20 yaliyokwama bandarini yakidaiwa kodi.
“Wananchi na vyombo vya habari wamejitolea na kuendelea kuhamasisha, huku walimu wakichanga kama sehemu ya kujikomboa, leo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameamua kuuza samani za walimu kwa wamiliki wa kumbi za starehe ili walimu waendelee kugombania madawati na vyoo na wanafunzi.”
“Mimi Paul Makonda nimefanya kwa sehemu yangu kilichobaki ni mwenye wazo atasimama siku moja kujitetea kwa sababu Mungu ndiye aliyewawezesha watu wakakubali kujitolea,” amesema.
Makonda alisema, “Nakuhakikishia atakayenunua hivi vifaa vya walimu amelaaniwa yeye na uzao wake na kamwe hatafanikiwa katika maisha yake. Nayasema haya nikiwa na uhakika kwa kuwa vya madhabahuni havichezewi.”
“Hivi ni vifaa kwa ajili ya walimu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mungu hakunipa kwa ajili ya baa wala kumbi za starehe,” alisema Makonda.
Juzi, Mwananchi ilifika kwenye mnada uliofanyika eneo la bandari kavu ya Malawi Cargo na kukuta ukikaribiwa kufungwa.
Ilidokezwa kuwa samani hizo zilikosa wanunuzi baada ya wateja kushindwa kufika bei ambayo mmoja wa wateja waliokuwapo eneo hilo alisema kila kontena lilikuwa likiuzwa kwa Sh60 milioni.
Kabla ya jana kutoa maelezo marefu kuhusu makontena hayo, juzi Makonda aliliambia Mwananchi kuwa hana taarifa ya kupigwa mnada kwa makontena hayo.
“Sina taarifa ya kupigwa mnada vifaa hivyo, mimi nipo msibani, ila kauli yangu kwa walimu ambao ninawajali na kuwapenda, wasikate tamaa, nawapenda sana, ujumbe wangu mkubwa kwao ni wamtegemeao Mungu ni kama Mlima Sayuni hawatatikisika kamwe,” alisema Makonda.
Tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, liliwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.
Tangazo hilo lilionyesha kuwa TRA inakusudia kufanya mnada wa wazi Juni kwa mizigo iliyokaa bandarini kwa muda mrefu bila kukombolewa, ikiwamo ya Paul Makonda.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye na kuchapishwa na Daily News, wamiliki walitakiwa kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.
Tangazo hilo lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na bidhaa kadhaa kama vile samani.
Ingawa hakukuwa na uthibitisho kuwa Makonda ndiye mwenye makontena hayo wakati huo, Februari 16 mkuu huyo wa mkoa alikaririwa katika mtandao wa gazeti la Serikali la Habari Leo kuwa alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa. Mzigo huo ulikuwa sehemu ya shehena ya makontena 36.
Samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni, zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.
Wakati huo huo, alipotafutwa na Mwananchi, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka ilitoa notisi ya siku 30 kwa waagizaji wa mizigo ambao mizigo yao imekaa bandarini kwa zaidi ya siku 90.
“Tangazo lililotolewa ni notice (taarifa) kwa wahusika ili wakomboe mizigo yao ndani ya siku 30. Isipokombolewa itanadiwa. Mizigo hiyo inaweza kuwa ni ile ambayo haijalipiwa kodi au hata ile iliyolipiwa lakini haijaondolewa,” alisema Kayombo alipozungumza na Mwananchi, Mei 17.
Alipoulizwa kama shehena hiyo ni mali binafsi ya Makonda au ya ofisi yake, Kayombo alisema: “Majina yaliyoandikwa kwenye magazeti ndiyo taarifa za consignees (wapokeaji) zilizo kwenye nyaraka. Madhumuni ya matumizi si sehemu ya wajibu wetu.”
Baadaye Mei 20 ilisambaa barua ya TRA, ikionyesha makontena ya Paul Makonda yana thamani ya Sh1.4 bilioni.
Barua hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilieleza kuwapo ombi la msamaha wa kodi wa mali hizo kutoka kwa Makonda kwenda kwa Waziri wa Fedha, Philip Mpango, maombi ambayo hayastahili kuridhiwa, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi.
Pia, barua hiyo ambayo si TRA wala Dk Mpango waliothibitisha kuitambua, iliandikwa na mamlaka hiyo ya ukusanyaji kodi kumueleza waziri husika kuwa ombi hilo haliwezekani kwa kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina sifa ya kupata msamaha kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya kupitia maombi hayo, tunapenda kukufahamisha kuwa sheria ya forodha ya Jumuia ya Afrika Mashariki ya 2004 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014 hazijatoa msamaha wa kulipa ushuru wa forodha na VAT kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa,” ilieleza barua hiyo.
Ilieleza kutokana na sheria hiyo, ofisi ya mkuu wa mkoa ni sehemu ya Serikali za Mitaa, hivyo haistahili kupata msamaha.
Barua hiyo ilitaja kiwango cha thamani ya mali hizo, ikirejea ombi la msamaha wa kodi lililowasilishwa na ofisi hiyo ya mkoa.
Kabla ya figisu hizo za msamaha wa kodi na tangazo la TRA, Februari Makonda aliwapeleka bandarini baadhi ya walimu wa jijini Dar es Salaam, waandishi wa habari na wadau wengine ambako aliwaonyesha makontena yenye vifaa vya ofisi na vya kufundishia, akisema vimetolewa na Watanzania waishio Marekani.
Hata hivyo, vifaa hivyo ambavyo baadhi ni viti, meza na mbao za kuandikia, vilionekana ndani ya makontena vikiwa vimeshaunganishwa, tofauti na hali ya kawaida ya kusafirisha bidhaa zikiwa hazijaunganishwa ili kuziweka nyingi kwenye kontena moja kwa ajili ya nafasi.