Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Makonda: Sijawatuma mgambo kuwapiga, kudhalilisha wananchi

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hajawatuma mgambo kupiga wananchi au kuwadhalilisha na wala hana nia mbaya katika kampeni ya usafi, bali anataka jiji hilo liwe safi.

Akizungumza jana wakati aliposhiriki kampeni ya usafi katika Kambi ya Jeshi Lugalo, alisema baadhi ya vijana wa mgambo wanaosimamia suala hilo wanalifanya kwa kuwapiga raia, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.

Makonda aliyasema hayo ikiwa ni siku mbili baada ya video kusambaa mitandaoni ikiwaonyesha mgambo wakimpiga kikatili mwananchi na nyingine ikionyesha mwanamke anayechuruzika damu usoni akidai mgambo hao wamempiga na rungu.

“Leo nimeamka, na gazeti la Mwananchi linasema mgambo wa Makonda wawapiga watu. Maana yake tafsiri nyepesi, Makonda ametuma mgambo wakapiga raia, jambo ambalo si kweli na wala halina mpango mwema katika kampeni hii,” alisema Makonda.

Makonda alisema endapo mtu mmoja akikosea au wawili, zipo taratibu na tayari amekwishaelekeza watu hao wamekamatwa na kuwekwa ndani huku taratibu za kinidhamu zikichukuliwa.

Juzi mara baada ya kusambaa kwa video hizo, kamanda wa Polisi Kinondoni, Jumanne Muliro alisema mgambo watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kumpiga na kumjeurhi mkazi wa Bunju A, Robson Orotho.

Akizungumza na wanajeshi Kambi ya Lugalo jana, Makonda alisema, “nilitegemea leo magazeti yangeandika ‘waliokiuka utaratibu wa kampeni ya usafi washughulikiwa’, hilo ndiyo ingekuwa headline (kichwa cha habari) nzuri ya kuonyesha jambo hili ni jema na kwa manufaa ya watu wote.”

Alisema viongozi wote waliopo mkoani Dar es Salaam yeye akiwa mkuu wao wanataka jiji liwe safi.

Makonda alisema kwa kuwa sheria zipo kila anayekiuka atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Watendaji wa mitaa ndiyo mabosi wa hawa mgambo kuhakikisha wananchi wanafanya usafi. Kupigwa siyo adhabu iliyoandikwa kwenye sheria, kwenye sheria imeandikwa faini na tuliamua kufanya hivyo baada ya kuondoa zuio la kila Jumamosi kufunga maduka.”

Malalamiko

Akizungumzia kadhia za mgambo hao, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mivumoni-Madale, Deodatus Kamugisha alisema juzi amewazuia kupita na kukagua takataka katika eneo hilo kwa sababu wamekuwa kama wezi.

Alisema badala ya kutoa elimu, wanawakamata wananchi kama majambazi na kuwatoza faini ya zaidi ya Sh70,000.

Kamugisha alisema juzi walikuwa na kikao cha maendeleo ya kata na alikuwa anakaimu nafasi ya udiwani ndipo alipopokea malalamiko kutoka kwa wenyeviti wa mitaa.

“Hawa mgambo wameambiwa kwa kila faini wanayowatoza wananchi wana asilimia, hivyo wanafanya kila hila kuhakikisha wanawabambikia kesi (wananchi) ili wawapeleke kwa mtendaji wakatiwe risiti na wao wapate fungu lao,” alisema.

Alisema amekataza utekelezaji wa majukumu ya mgambo hao kwa sababu ameona hawafai na kama kuna kesi ya kujibu kwa mkuu wa mkoa yuko tayari kuijibu.

Kamugisha alisema wenyeviti hawapingi shughuli ya usafi kwa sababu ni njema, lakini inahitajika elimu zaidi kuliko kutumia nguvu.

Alisema ili waunge mkono suala hilo magari ya kukusanya taka yawepo na wanaotozwa faini wapewe risiti za kielektoniki (EFD).

Hukumu ya kipigo

Akizungumzia ‘hukumu ya kipigo’ inayotolewa na mgambo hao, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema sheria haiwapi mamlaka mgambo wala askari wa aina yeyote kuwapiga raia.

Alisema mtu akikiuka sheria iwe ya kutofanya usafi, kutolipa faini ya kosa hilo inaelekeza akamatwe na kupelekwa mahakamani kwa kufanya kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act).

“(Mtu) hatakiwi kupigwa hata kama anakataa kutii sheria, akizidi matata afungwe pingu apelekwe polisi ambako pia hapaswi kupigwa,” alisema Henga. “Sehemu pekee anakopaswa kupata adhabu ni mahakamani ambapo siku hizi adhabu za viboko zimeondolewa, badala yake atahukumiwa kifungo au kutozwa faini.”

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa alisema tabia ya kupiga ovyo mgambo wameiiga kutoka kwa polisi ambao wamekuwa wakifanya hivyo kila mara.

Alisema sasa kila mwenye madaraka anaona afanye hivyo na hata walimu katika miaka ya hivi karibuni wameiga ndiyo maana ya kuwapo kwa matukio mbalimbali ya kuwajeruhi wanafunzi na hata kusababisha vifo.

“Hatukatai watu kutozwa faini kwa kukiuka sheria na taratibu, suala la usafi ni zuri na linahitaji msukumo hususan kwenye jiji kubwa kama Dar es Salaam, lakini namna linavyotekelezwa ndiyo lina kasoro kubwa,” alisema.

“Turudi nyuma, walinzi wa usalama wa raia wapatiwe elimu ya jinsi ya kutimiza majukumu yao, tofauti na hapo nchi itakuwa ya vilio kila kukicha.”

Sakata lilipoanzia

Sakata hilo lilianza baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi na baadaye video zilizosambaa kwenye kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha mgambo wanaosimamia operesheni hiyo iliyoasisiwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda wakiwapiga wananchi na wengine kulalamika kujeruhiwa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, Makonda alitangaza kuanzisha operesheni ya usafi akisema itashirikisha askari 400 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi.

Chanzo: mwananchi.co.tz