MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amewaondoa hofu wafanyabiashara wa soko dogo Kariakoo maarufu soko la mabati, kwamba kuondolewa kwao eneo hilo ni kwa ajili ya kufanya ukarabati pamoja na ujenzi.
Amesema ni kuboresha mazingira ya kufanyia biashara.
Alisema juzi kuwa wafanyabiashara hao wanatambuliwa na hawamo kwenye orodha ya makundi matano yanayohamishwa ikiwamo wanaofanyia biashara maeneo yasiyo rasmi.
Makalla aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Nipashe, kujibu suala la wafanyabiashara wa soko hilo ambao juzi wakidai wanahamishwa eneo hilo bila kupewa taarifa za awali.
“Wafanyabiashara wa soko dogo hawako katika makundi matano yanayotakiwa kuhama. Siyo waliopo kwenye 'road reserve' (hifadhi ya barabara), mitaro, njia ya wapita kwa miguu, mbele ya maduka wala kwenye taasisi za umma.
“Hawahamishwi kama wamachinga ila watahamishwa kupisha ujenzi wa soko kwa faida yao wao,” alisema Makalla.
Juzi, wafanyabiashara wa soko dogo la Kariakoo takribani 1,000 wakizungumza na waandishi wa habari, walidai kwamba, uongozi wa mkoa umewapa muda mfupi kabla ya kuondolewa eneo hilo, wakidai siku 10 walizopewa, hazitoshi.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko dogo la Kariakoo Dar es Salaam, Hussein Magae, alisema wameshangazwa na uamuzi wa kwamba waondoke eneo hilo haraka, bila kuzingatiwa idadi yao, akisema wapo sokoni hapo kisheria.
Magae aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari sokoni hapo, kuhusu kutakiwa kupisha ujenzi wa jengo la ghorofa nane.
Alisema wakiwa kama wadau wa maendeleo na wanaofanya biashara kwenye eneo lililothibitishwa kisheria ikiwamo kulipa kodi, ni vyema washirikishwe katika kila hatua ya kuendeleza soko hilo.
“Kuna taarifa kwamba soko hili dogo kunatakiwa kujengwa jengo la ghorofa la nane. Tuko zaidi ya 1,000 iweje tupewe siku chache,” alisema Magae.
Mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, Arcardo John alisema ni kawaida yanapofanyika mabadiliko hutolewa taarifa mapema na kwamba wanafanya biashara eneo hilo kwa mujibu wa sheria kutokana na kulipa kodi.