MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amewataka wamachinga walioweka vibanda vyao juu ya mitaro katika eneo la Bunju kuviondoa ili kuepusha uzibaji wa mitaro hiyo na kutoa mwanya kwa wasafishaji kusafisha vizuri mitaro hiyo.
Alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali katika Wilaya ya Kinondoni ikiwemo Hospitali ya Mabwepande ambapo alisema serikali haipo tayari kuona uharibifu ukifanyika katika mitaro hiyo.
Alisema serikali imeshatenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya biashara na wafanyabiashara hao ni vyema wakaenda katika ofisi za kata kwa ajili ya kupewa utaratibu uliopangwa na kupitia maelekezo yaliyo kwenye kitabu chake alichokizindua Septemba 17, mwaka huu na siyo kuvamia maeneo yasiyo rasmi, suala linalosababisha usumbufu usio wa lazima.
"Serikali ina nia nzuri na nyie wote mliojenga kwenye mitaro kama hapa angalieni kote mnapoweza kukaa na kufanya biashara zenu, hapa sio sehemu sahihi ya nyie kufanya biashara... Kupitia watendaji wenu nimewaelekeza waje kuwapanga na kuwapeleka sehemu husika lakini siyo hapa," alisema.
Alisisitiza kwamba, kufanya biashara katika maeneo hayo kuna madhara mengi yakiwepo ya kutuwama kwa maji na hivyo kusababisha usumbufu kwa watu wa maeneo hayo.