Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amekutana na kufanya mkutano na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo baada ya maandamano yaliyotokea leo asubuhi, wafanyabiashara hao wakishinikiza kukutana na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya madai yao ya kutaka kupunguziwa kodi wanazotozwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Akizungumza na wafanyabiashara hao, RC Makalla amesema kuwa wao kama Serikali wamepokea malalamiko hayo na wanatambua umuhimu wa Soko hilo.
Makalla amewataka wafanyabishara hao kuendelea na biashara hizo, baada ya wafanyabishara hao kugoma kufungua biashara hii leo.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa naelewa umuhimu wa Kariakoo, tuko watu mbalimbali hapa na tunategemea, Kuna watu maduka yakifungwa hapa kariakoo hawana tena kazi.
“Sioni sababu ya kufunga biashara. Viongozi wetu wanazungumza na Serikali na Waziri Mkuu, na makubaliano yatafikiwa,” amesema, Makalla.