Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema Mkoa wa Lindi ndio unaoongoza kwa kufaulisha wanafunzi wa kidato cha sita katika shule za sekondari nchini.
Ameongeza kuwa mkoa huo umeongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia tisa mwaka 2012 hadi kufika asilimia 35 mwaka 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi alipokuwa akifungua rasmi mafunzo ya mradi wa shule salama za Sekondari (SEQUIP) yaliyofanyika katika Manispaa ya Lindi, Ndemanga amesema mkoa huo umefanikiwa kufuta daraja la sifuri (Division 0 na IV) kwa kidato cha sita na kwa sasa alama za ufaulu ni daraja la kwanza, la pili na wachache sana daraja la tatu.
Ndemanga amesema malengo ya mkoa wa Lindi ni kwenda na mwendo huo hadi kwa kidato cha nne kwani hadi sasa baadhi ya wilaya za mkoa huo zimeanza kufuta daraja la sifuri akiitaja Wilaya ya Liwale kuwa moja ya wilaya hizo na kwamba kwa wilaya zingine daraja sifuri zimepungua idadi kutoka 400 hadi 40.