Mkuu Wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amekemea vikali vitendo vya ukatili vinavyoendelea kushamiri ndani ya jamii na kusema mwanamke Neema John(Mmangati), aliyefanyiwa ukatili na mume wake kwa kupigwa na bakora mgongoni pamoja na kumwagiwa maji ya Moto kisha kukimbia kusikojulikana asakwe ili vyombo vya sheria vichukue hatua.
Akielezea juu ya tukio hilo, Kunenge alisema yapata siku ya kumi mwanamke huyo,mkazi wa Kwala kufanyiwa unyama huo ,na kuachiwa majeraha makubwa na maumivu makali ambapo ameachwa na watoto wanne akiwemo mtoto mchanga wa siku 26. Aliitaka ustawi wa jamii mkoa kulibeba suala hilo,wafuatilie Mazingira aliyoachwa nayo mwanamke huyo,na Watoto wake baada ya tukio hilo na kumsaidia Hadi atakapokuwa sawa.
“Vitendo hivi ni vya hovyo kabisaaa, huyu ni muuuaji kumpiga mkeo namna ile,ni kwamba alidhamiria kumuua, vyombo vya sheria vimsake na kuchukua hatua” Mkuu huyo wa mkoa,alitoa rai kwa wanawake na jamii kuacha kuficha vitendo na viashiria vya aina hiyo ili kuokoa maisha, kupata matibabu haraka na pia iweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mhusika.
Kunenge aliwataka viongozi wa dini, Serikali,kijamii, vyama vya siasa, kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kuhusiana na kuacha vitendo hivi vya ajabu ambavyo haviendani na sera, sheria,kanuni na mila na desturi za nchi yetu.
Hata hivyo aliwaasa watendaji wa ustawi wa jamii pamoja na mkoa kuacha kukalia taarifa za aina hiyo, wazitoe kwa wakati pasipo kuficha ofisi yake ili zifanyiwe kazi.
“Haiwezekani vitendo hivi vinatokea, taarifa mnazipata mitandaoni,mtu anapelekwa Kituo Cha afya Mlandizi,Tumbi, Serikali hamjui,mnasubiri kutumiwa picha mitandaoni, haiwezekani, mnasubiri mkuu wa mkoa ndio nifuatilie wajibu wenu,” “Mimi nitashughulikia mambo mangapi,kwahili nitawashughulikia na kuwajibisha wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine”Inakera yaani Rc nitoke ndio nishughulikie wajibu wenu, atakaekuwa kabainika kuhusika nitamwajibisha.”alifafanua Kunenge.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Pwani Pius Lutumo alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema bado mhusika hajapatikana ,jeshi la polisi linaendelea na msako “Ujue hawa wafugaji huwa wanatabia ya kufanya tukio na kukimbilia maporini ,Lakini licha ya Hilo tupo kazini na Tutahakikisha tunamkamata “alisisitiza Lutumo.
Lutumo aliitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, na wenye ndoa kuacha kupiga na kufanyia ukatili wenzao wao kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa haki ya binadamu.
Kwa upande wake,Neema John akiwa hospital ya rufaa ya mkoa ya Tumbi kwa matibabu alieleza anashukuru kupata matibabu na anaendelea vizuri kidogo. “Kosa langu lilikuwa kuchelewa kuwasha moto ndipo mume wangu kuamua kunipiga kiasi hiki mgongoni,usoni na kunimwagia maji ya Moto mapajani,na mguuni”alieleza Neema.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani Gunini Kamba, alieleza Neema alipokelewa akitokea Mlandizi lakini sasa anatibiwa Hospital ya Tumbi na wanashukuru anaendelea na matibabu.
Kaimu mganga mkuu mfawidhi hospital ya rufaa ya mkoa Tumbi,Dkt Devotha Julius alisema Neema kiafya anaendelea vizuri,yupo kwenye matibabu.
Akielezea hali ya Mapokezi ya wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo kutokana na unyanyasaji na ukatili kwa wanawake na watoto alisema ,wanapokea wagonjwa wa aina hiyo watatu hadi wa nne kwa mwezi.