WATANZANIA wametakiwa kuchukua tahadhari na watu ambao wanatoa lugha za uchonganishi na ubaguzi zenye lengo la kuvuruga amani ya nchi
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba wakati akifungua warsha ya uelimishaji wa umma kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 Mkoani humo.
Rc Kindamba amesema zoezi hilo litasaidia kujenga uelewa kwa viongozi kuanzia ngazi ya Mkoa, wilaya na Halmashauri kuhusu mchakato wa maandalizi ya dira ya maendeleo ya 2050 ambapo amewataka wananchi kuwapuuza wale wote wenye nia ovu kuhusu zoezi hilo.
“Hiki tunachokifanya Leo kitakuwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Tanzania tuitakayo mwaka 2050 hivyo mpango huu sio Kwa ajili ya kundi fulani bali tutoe maoni yetu Kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu na sisi wananchi wenyewe”amesema RC Kindamba.
Nae Mwenyekiti kamati ya uandishi dira ya Taifa ya maendeleo 2050 Gladness Salema amesema kuwa zoezi hilo ni la kimkakati hivyo lazima kazi hiyo ifanyike kwa uaminifu na uadilifu.