Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Kilimanjaro ageuka mbogo ujenzi wa madarasa

Rcmoshipic Data RC Kilimanjaro ageuka mbogo ujenzi wa madarasa

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya uchunguzi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika manispaa ya Moshi vilivyogharimu Sh80 milioni.

Kagaigai ametoa siku saba kwa taasisi hiyo, kuhakikisha inakamilisha uchunguzi huo wa kina ikiwa ni pamoja na kuchunguza mikataba ya ujenzi ili kuona kama thamani ya fedha inalingana na hadhi ya jengo.

Vyumba hivyo ni miongoni mwa vyumba 22 vinavyojengwa manispaa ya moshi chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano ya Uviko 19.

Kagaigai ametoa agizo hilo jana Alhamisi Desemba 16, 2021  wakati kamati ya usalama ilipofanya ukaguzi wa Majengo hayo ambayo yalistahili kukamilika Desemba 15, 2021 na baadae serikali kuongeza muda wa wiki mbili hadi Desemba 31, 2021

"Ile milango ile ni mipya? Enjinia kwenye kitasa umeona? Mbona unamtetea sasa yaani iko wazi kabisa vitu viko hovyo kabisa halafu unatetea?" amehoji Mkuu wa Mkoa akionyesha kukerwa na majibu aliyokuwa akipewa ya ujenzi huo.

"Heshimu na taaluma za watu wengine na watu waliokuja kukagua, usidhani kuwa uinjinia ndio kujua kila kitu," amesema Mkuu wa Mkoa.

"Nielekeze marekebisho haya yafanyike haraka na niitake Takukuru waendelee kufanya ufuatiliaji na uchunguzi kwa ajili ya kubaini haya ni kwa nini yametokea na Mkuu wa Wilaya mpite madarasa yote kukagua kabla hayajakabidhiwa"

"Kamanda wa Takukuru nakupa siku saba uniletee taarifa za ukaguzi utakaofanya Shule hizi mbili lakini pitia na nyingine ili kujiridhisha kwani sijaridhishwa na jinsi Kuta, sakafu na milango ya darasa, " alisisitiza mkuu huyo wa mkoa.

Akizungumza mbele ya msafara huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Seif Shekalaghe amewataka wasimamizi wa halmashauri kusimama kwenye nafasi zao na kuepuka kujiingiza sehemu za wataalamu.

"Mapungufu yaliyobainika hapa ni makubwa halafu ninyi mnasema ni madogo madogo, hii milango ni mibovu hivyo ni lazima tusikilize wataalamu wanatuambia nini lakini na wale ambao ni wasimamizi wasijiingize kwenye utaalamu,"alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz