Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Kijuu amefanya mengi Kagera, pia kaacha viporo mezani

9536 Pic+kiju TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukituminya na sisi tunakuminya. Hii ndiyo kauli itakayokumbukwa zaidi na waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera. Mara chache walipata fursa ya kuuliza maswali kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu.

Ni jibu alilopewa mmoja wa waandishi aliyehoji chombo anachowakilisha kutokuwa kwenye orodha ya vile vitakavyoshiriki ziara ya kiserikali. Majibu yake yalikuwa ni mafupi na mazito na hakuwa aina ya kiongozi anayependa kusikika sana.

Aina yake ya uongozi ilijipambanua ukilinganisha na watangulizi wake kwa kutoa maelekezo na kufanya ufuatiliaji kimyakimya. Hakuwa kiongozi wa matangazo sana pengine utumishi wake jeshini ndio uliomfanya aonekane kiongozi wa kutoa uamuzi kuliko kutawaliwa na siasa.

Kuna mambo ambayo mpaka leo yasingetekelezeka kama angeruhusu kuingiliwa na ushawishi wa wanasiasa ambao huangalia zaidi masilahi ya wapigakura wao kwa kipindi wanachoongoza kuliko kuangalia mambo ya kesho.

Mkuu huyo wa mkoa anaondoka ofisini akiacha mambo mazito mezani.

Huyu ndiye mkuu wa mkoa wa pili aliyekuwa na mzigo wa kuongoza shughuli za uokoaji wakati wa maafa ya tetemeko la ardhi baada ya Mohamed Babu kufanya kazi kama hiyo wakati wa maafa ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba 1996.

Alivyowakabili wafugaji

Wafugaji ni miongoni mwa makundi yanayoaminika kuwa na ushawishi kwenye ngazi mbalimbali za uongozi, hasa kwa wanasiasa. Nguvu yao ya kushawishi na kutengua misimamo ya baadhi ya viongozi huusishwa na uwezo wao wa kumiliki uchumi.

Uondoaji wa mifugo na wafugaji katika maeneo yaliyotengwa kisheria lilikuwa ni tatizo sugu mkoani Kagera ambapo juhudi za kuwaondoa ziligonga mwamba mara zote. Baadhi ya watendaji waliosimamia sheria za uhifadhi walijikuta wanapata onyo lilitokana na shinikizo la kisiasa.

Suala la kuwaondoa wafugaji kwenye mapori ya Biharamulo, Buligi na Kimisi tayari lilishapewa hadhi ya kushindikana. Kilichotisha zaidi hata Kamati za Bunge zilizotembelea maeneo hayo na kushuhudia uharibifu uliopo, lakini walipofika bungeni nguvu kubwa ilikuwa ni kutetea wafugaji.

Meja Jenerali Kijuu alifanya ziara katika maeneo hayo na kuhitimisha ziara yake kwa kutoa muda kwa mifugo kuondolewa katika maeneo hayo. Ilikuwa ni kama aina ya vitisho ambavyo vilishazoeleka kutoka kwa watangulizi wake.

Haikuwa kama walivyofikiri, kilichofuata ni operesheni kali ya kuwaondoa ambayo haikuwahi kushuhudiwa kabla ya hapo. Pamoja na changamoto zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo hakutoa nafasi ya kurudishwa nyuma.

Matokeo ya usimamizi wa zoezi hilo ilikuwa ni kuanza kurejea kwa wanyama pori ambao walishindwa kuhimili ushindani wa maeneo ya malisho na makundi makubwa ya wafugaji baadhi yao wakidaiwa kutoka nje ya nchi.

Matokeo makubwa zaidi ilikuwa ni Rais John Magufuli kuridhia maeneo hayo kupandishwa hadhi na kuwa Hifadhi za Taifa. Kwa sasa yametulia na hatua hiyo itawezesha maeneo hayo kuchangia zaidi uchumi wa nchi kupitia shughuli za utalii.

Akipongeza hatua ya mkuu huyo wa mkoa, Rais John Magufuli alisema zoezi limeendeshwa kwa mafanikio makubwa na kutaka liwe endelevu na kutaka mkuu huyo wa mkoa asilaumiwe huku akionya watakaoendelea kukaidi sheria.

Wawekezaji wa wamshangaa

Wiki chache kabla ya kustaafu, Meja Jenerali Salum Kijuu amefanya ziara katika ranchi ya Kagoma ambapo wawekezaji wamepewa maeneo makubwa ya kulisha mifugo na kujikuta kwenye migogoro na wananchi.

Kilichowashangaza wawekezaji hao ni kukataliwa kwa ombi lao la kutaka Serikali itumie nguvu kuwaondoa wananchi waliopo kwenye maeneo yenye migogoro kwa kuwa tayari wameshinda kesi mahakamani dhidi ya wananchi.

Badala yake, Kijuu aliwaeleza kwamba anafahamu kuwa wawekezaji hao wameshinda kesi dhidi ya wananchi, lakini Serikali haiwezi kutumia nguvu kubwa kuwaondoa kwenye maeneo wanayomiliki kisheria kwa kuwa hautakuwa mwisho wa mgogoro.

Baadhi ya wawekezaji waliomba waruhusiwe hata kugharamia zoezi la kuwaondoa wananchi wanaotuhumiwa kuvamia maeneo ya uwekezaji, hatua iliyokataliwa pia, akisema Serikali inatafuta njia za busara zaidi.

Pamoja na baadhi yao kusema watasita kulipa baadhi ya tozo za vitalu kwa kuwa so maeneo yote waliyopewa wanayatumia kama walivyoomba baada ya kuvamiwa na wananchi, bado haikusaidia kubadili msimamo wa RC Kijuu kuwa inahitajika busara zaidi.

Magendo ya kahawa

Tatizo la udhibiti wa magendo ya kahawa sio kwamba mzizi wake haukujulikana bali watuhumiwa wa biashara hiyo pia waliruhusiwa kuwa sehemu ya vikao vya uamuzi, jambo lililodhoofisha juhudi za udhibiti.

Suala la kudhibiti magendo ya biashara ya kahawa havikuhitaji ushiriki wa wanasiasa ambao wanalinda masilahi ya wapiga kura, jambo lililomfanya RC Kijuu kutoa maelekezo ya moja kwa moja.

Wakati akizindua zoezi la ukusanyaji wa kahawa kupitia mfumo mpya wa stakabadhi ghalani, RC Kijuu alionya kuwa wananchi watakaojihusisha na magendo ya kahawa wasije kujutia baadaye na akataka watoe ushirikiano wakati wa zoezi hilo.

Ndivyo ilivyo sasa, hatua kali zilizofuata baada ya hapo zimefanya biashara hiyo kuwa ngumu zaidi ikilinganishwa na miaka mingi iliyopita ambayo haikuwa rahisi kushuhudia magari yaliyokamatwa na kuchukuliwa na Serikali.

Wavuvi hawako salama

Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu huku wavuvi wakiminywa kwa matumizi ya nyavu haramu, diwani wa Kata ya Miembeni, Richard Mwemezi alipeleka kilio hicho kwenye Baraza la Madiwani wa Bukoba.

Katika kilio chake diwani huyo alidai kushangazwa na ukimya wa mkuu wa mkoa katika kipindi ambacho wavuvi wa eneo la Nyamukazi walikuwa wanachukuliwa vifaa vyao vya uvuvi bila Serikali kuingilia.

Haya yalikuwa ni maoni ya mwanasiasa ambaye alikuwa anabeba wajibu wa kuwatetea wapiga kura wake kama inavyofanyika katika maeneo mengine na kwake hatua ya kumlaumu kiongozi wa Serikali, hakuna kitu alichokuwa anapoteza.

Badala ya kumjibu kisiasa, Mkuu wa mkoa aliitisha mkutano katika eneo la wavuvi waliotetewa na diwani na baada ya kusikiliza malalamiko yao alitoa nafasi kwa wataalamu kutoa majibu.

Hakuna lililobadilika, operesheni ya kuwadhibiti iliendelea huku wanasiasa wakilalamika kimyakimya kuwa wanaonewa ambapo alisisitiza kuwa ulikuwa ni utekelezaji wa sheria inayolenga kuokoa rasilimali za ziwa.

Viporo mezani

Kila kiongozi ana mtindo wake wa kutekeleza mambo anayoamini na katika hatua hii yapo mambo yanayoachwa na Kijuu ambayo huenda yakapata msukumo mpya au yakafia mezani na kuibuliwa mapya.

Uwekezaji wa kilimo cha mpunga katika mabonde yaliyopo mkoani Kagera ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyofikiliwa na Meja Jenerali Salum Kijuu ambaye mpaka anastaafu hakuna dalili za mradi huo kuanza.

Katika moja ya vikao alivyoendesha kama mwenyekiti, alilalamikia juhudi zake kukwamishwa na mmoja wa vigogo waliopo kwenye Wizara ya Kilimo na kushangaa ucheleweshwaji wa mradi huo ambao tayari umeonesha mafanikio upande wa Zanzibar.

Ndoto yake alikuwa anataka kuona Mkoa wa Kagera unalisha mikoa mingine na kuwa na ziada ya kuuza hata kwenye nchi za nje kutokana na rasilimali ya ardhi na hali ya hewa na kuwa amefanya ushawishi mkubwa wa kumleta mwekezaji ambaye bado alikuwa hajapata kibali.

Pia, Mkuu wa Mkoa anayechukua nafasi yake Brigedia Jenerali Gaguti anategemewa kuendeleza juhudi zilizoanza za ujenzi wa chuo cha kipekee cha ufundi katika eneo la Burugo Wilaya ya Bukoba.

Chuo hicho ambacho Meja Jenerali Kijuu ameongoza juhudi za kuhakikisha kinaanza haraka, tayari eneo husika limekaguliwa na wataalamu kutoka China, nchi ambayo inatarajiwa kuwekeza zaidi ya 21 bilioni katika mradi huo.

Ni hatua kubwa ambayo Kijuu alisema itasaidia kuwanoa vijana kutoka maeneo ya Kanda ya Ziwa ili kufanikisha azima ya Serikali ya viwanda.

Katika mapokezi, wawekezaji hao walisema vijana watanolewa hata katika matumizi ya teknolojia.

Kampeni yake ya kupanda miti ya matunda kwenye mji wa Bukoba ambayo tayari imeungwa mkono na wadau mbalimbali na utekelezaji kuanza haitegemewi kufia kwenye mikono ya Brigedia Gaguti.

Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, Meja Jenerali Salum Kijuu anastaafu na kuondoka Kagera bila jibu la kwanini eneo lenye rasilimali nyingi kiasi hiki kuendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuwa masikini zaidi nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz