Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Kigoma akumbushia maagizo ‘yaliyolala’ tangu 2016

10469 Pic+maigizo TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga amewaapisha wakuu wawili wa wilaya huku akitoa maagizo kadhaa, yakiwemo aliyoyatoa mwaka 2016 ambayo hadi sasa hayajatekelezwa.

Wakuu wa wilaya walioapishwa leo Jumatatu Agosti 6, 2018 ni Kanali Simon Hanange wa Kasulu na Luteni Kanali Michael Ngayalina wa Buhigwe huku akiwataka wazingatie sheria, kanuni na miongozo katika kutekeleza majukumu yao.

"Kuna maelekezo nilitoa tangu mwaka 2016 nilipoletwa kuwa mkuu wa mkoa Kigoma lakini hadi sasa hayajafanyiwa kazi kikamilifu, nendeni mkayatekeleze pamoja na maagizo mengine aliyotoa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alipokuja hapa wiki iliyopita," amesema Maganga.

Baadhi ya maagizo hayo ni kila halmashauri kuanzisha kituo cha matrekta ili wakulima waweze kukodi kwa ajili ya kilimo na kuachana na kilimo cha jembe la mkono.

Pia, aliagiza ulinzi kuimarishwa  katika mitaa na vijiji kwa kuanzisha mpango wa nyumba kumi za kiusalama katika kila eneo wanapoishi watu kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Amewataka wakuu hao wa wilaya kufuatilia halmashauri zao kuona namna wanavyokusanya mapato kutoka vyanzo vya ndani kwa kuwa makusanyo yamepungua hasa katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Wakizungumza baada ya kuapishwa Kanali Hanange amesema atashirikiana na wananchi wa Kasulu kuhakikisha rasilimali zilizopo zinaleta maendeleo katika wilaya, mkoa na Taifa.

Kwa upande wake Luteni Kanali Ngayalina amesema ameletwa katika wizara hiyo kumsaidia Rais John Magufuli kusukuma gurudumu la maendeleo mbele, kuomba ushirikiano wa dhati kutoka kwa viongozi wenzake.

Chanzo: mwananchi.co.tz