Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Kigoma aagiza wahamiaji haramu wakamatwe, wafungwe

10472 Pic+wahamiaji TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga ameiagiza Idara ya Uhamiaji kuanza msako wa kuwakamata wahamiaji haramu waliojificha kwenye mashamba na majumbani.

Ametoa agizo hilo leo Jumatatu Agosti 6, 2018 wakati akiwaapisha wakuu wa wilaya ya Kasulu na Buhigwe.

Amesema wahamiaji haramu mkoani humo wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili wahukumiwe kifungo.

"Watakaobainika kuvunja sheria wafungwe na huko wakafanye kazi hasa katika kipindi hiki cha kufufua mashamba ya michikichi, siyo wakakae tu na wakimaliza kifungo warudishwe katika nchi zao," amesema.

Ameiomba mahakama kuhakikisha kesi zote za wahamiaji haramu zinapewa kipaumbele ili kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani, ambao wanakula chakula bila kuzalisha.

Amesema kuna wahamiaji haramu na wakimbizi waliotoroka kambini wanaishi mitaani na kwenye nyumba za wananchi kinyume cha sheria, jambo ambalo halikubaliki.

"Katika hili hakuna siasa kama kuna kiongozi yeyote wa kisiasa anawalinda watu hawa ili wampigie kura kipindi cha uchaguzi shauri yake. Tutasimamia sheria," amesema Maganga.

Alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi kwamba si kila mtu mwenye hati ya kusafiria au kitambulisho cha kupiga kura atapata kitambulisho cha Taifa.

Licha ya matukio ya uhalifu kupungua mkoani Kigoma, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha uhalifu unakoma mkoani humo.

Chanzo: mwananchi.co.tz