Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Kebwe awasimamisha kazi maofisa wawili

51798 RC+PIC

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amesikitishwa na tabia ya baadhi watendaji kuomba rushwa kwenye miradi inayoendelea mkoani hapa.

Kutokana na hali hiyo, Dk Kebwe amewasimamisha kazi kaimu mganga mkuu wilaya ya Morogoro, Dk Kazimir Subi na ofisa ununuzi, Emmanuel Ntatie kwa tuhuma zinazohusiana na kukiukwa na maadili ya utumishi wa umma.

Maofisa hao wanatuhumiwa kuhusika na kuomba rushwa kwa baadhi ya mafundi wasimamizi waliopewa tenda ya ujenzi kwa ajili ya Kituo cha Afya Dutumi.

Mkuu huyo wa mkoa amechukua hatua hiyo leo Alhamisi Aprili 11,2019 baada ya kutembelea kituo hicho na kuelezwa kero mbalimbali zilizopo kutoka kwa mafundi waliokuwa wakiendelea na ujenzi, baadhi yao walimlalamikia mkuu huyo kuombwa rushwa ya Sh500,000 kwa kila jengo.

Dk Kebwe ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha inafanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na wampe taarifa.

Wakati huohuo, mkuu huyo wa mkoa ametoa siku 12 kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Kayombe Ryoba kuhakikisha ukamilishwaji wa ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Mkuyuni ambacho kimechukua muda mrefu kinakamilika.

Dk Kebwe akiwa katika ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo wilayani humo ikiwamo vituo vya afya Mkuyuni, Dutumi, hospitali ya wilaya na shule za msingi za Dutumi  na Mbwade ambazo majengo yake yaliezuliwa na upepo, amesema muda mrefu amefuatilia ujenzi wa vituo haridhiki na maendeleo yake.

Amesema mpaka Aprili 20,2019 ujenzi wa majengo ya kituo cha Mkuyuni yawe yamekamilika.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Ryoba akitetea kusuasua kwa ujenzi huo amesema changamoto iliyosababisha kuchelewa ni kutokana na usimamizi ambao haukuwa thabiti kipindi cha nyuma na kwamba kufikia Aprili 20 utakuwa umekamilika.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz