Biharamulo. Maofisa watatu wa halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera wamesimamishwa kazi na mkuu wa Mkoa huo Brigadia Jenerali Marco Gaguti.
Amechukua uamuzi huo ili maofisa hao wapishe uchunguzi wa upotevu wa zaidi ya Sh600 milioni ambazo hazikuwakilishwa kama mapato ya halimashauri kuanzia 2016 hadi 2018.
Hayo yamebainika jana Ijumaa Agosti 17, 2018 katika kikao maalum cha Kamati ya fedha na mipango ya halmashauri hiyo cha kujadili taarifa ya kamati iliyoundwa na aliyekuwa mkuu wa Mkoa huo.
Waliosimamishwa kazi ni Alexander Bashaula ambaye ni mweka hazina wa halmashauri hiyo, Salanga Mahendeka (mhasibu) na Emanuel Maleo ambaye ni ofisa ushirika, wote wakituhumiwa kupoteza fedha na kukiuka viapo vya uaminifu.
Katika kikao hicho mkuu huyo wa Mkoa amesema zaidi ya Sh690 milioni hazikuwasilishwa kama mapato ya halmashauri kuanzia Agosti 2016 hadi Mei 2018, Sh 427 milioni hazikuwasilishwa benki na wakusanya mapato.
“Baada ya uchunguzi wa kamati ya katibu tawala wa mkoa wa Kagera hivi karibuni ilibainika kuwa mwenendo wa ukusanyaji wa mapato haulidhishi na tunachukua hatua kwa wanaopoteza fedha za umma” alisema.
Ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kuchunguza ubadhilifu huo wa mali ya umma pamoja na kufuatilia wote kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.