Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge amemtaka katibu wa Chemba ya wenye Viwanda, Wafanyabiashara na Kilimo (TCCIA) mkoani humo, Rwechungura Mali kutopandisha bei ya vifaa vya ujenzi wakati ambao Serikali imetoa fedha za Uviko-19, Sh20 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 881 mkoani Kagera.
Ameyasema hayo akiwa katika mkutano na wakuu wa shule za sekondari na watendaji wanao simamia ujenzi katika Manispaa ya Bukoba na baadhi ya wafanyabiashara wanaopata tenda za ujenzi na vifaa.
Amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wameanza kuongeza bei ya bidhaa, akitolea mfano wilaya ya Missenyi ambako baadhi ya wafanyabiashara wa saruji wameongeza bei ya mfuko wa sementi kutoka Sh21,000 hadi kufikia Sh23,000.
Kutokana na hali hiyo amesema amemuita katibu wa wafanyabiashara ili ashiriki kwenye kikao hicho pamoja na watendaji wakuu wa wilaya hiyo ili kujua kama ndiyo wanawashawishi wafanyabiashara waongeze bei na kusema hawana nafasi.
"Haiwezekani bei ya saruji ilikuwa Sh21,000 halafu muda mfupi inapanda na kufikia Sh23,000. Nakuagiza katibu wa wafanyabiashara ongea na wafanyabiashara wako, hapa hatuna nafasi ya kuongeza bei,” amesema Meja Jenerali Mbuge.
Amesema jana alitembelea shule za sekondari za Ijuganyondo na Kagemu na kukuta mafundi wanalalamika kuwa ni siku ya nne hawajalipwa kwa kuwa mkuu wa shule alikuwa Manispaa akifuatilia hundi.
Aidha, Meja Generali Mbuge amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwa umekamilika ifikapo Novemba 30, 2021.
Naye katibu wa TCCIA Mkoa wa Kagera, Rwechungura Mali amekubali agizo hilo akiwataka wafanyabiashara wenzake kutopandisha bei ya vifaa vya ujenzi.