Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amemtaka mkandarasi wa barabara ya Bugene-Burigi Chato kilometa 60, kufanya kazi ndani ya muda aliopewa na kuimaliza kwa wakati.
Chalamila alifanya ziara wilayani Karagwe na kufanya ukaguzi wa barabara hiyo ambayo inaunganisha nchi za Tanzania, Uganda na Rwanda kwa Wafanyabiashara wanaotokea Kyerwa, Karagwe na Sudan Kusini.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha mawasiliano katika nchi nyingi, ambazo zinauzunguka mkoa wa Kagera, ikiwa ni pamoja na kurahisisha utalii katika hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato.
Katika ziara hiyo alimtaka msimamizi wa mradi huo, TANROAD Engneering Consultanting Unit (TECU) kumsimamia mkandarasi huyo, ili afanye kazi hiyo ndani ya muda wa miezi 30 aliopewa.
“Hii ni barabara ya kilometa 120 ila mpaka sasa wameanza na kilometa 60, barabara hii itakuwa na gharama ya jumla ya Sh bilioni 109 na inatakiwa ikamilike ndani ya muda wa miezi 30.
“Mpaka sasa mkandarasi ameshatumia miezi saba na mkandarasi yupo nyuma kidogo ya asilimia alizotakiwa kuwa amefanya kazi, hivyo sisi tunamsisitiza aongeze kasi, ili kuendana na muda aliopewa,” alisema Chalamila
Pia amewaelekeza Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Karagwe kuwawajibisha watu wanaoiba vifaa vya ujenzi vya barabara hiyo na kutoa onyo tabia hiyo ya wizi isijirudie tena.
Pia amemtaka Meneja wa Tanroad na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karagwe kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote wanaochimba mchanga eneo la hifadhi ya barabara.
Barabara ya Bugene-Burigi Chato kilometa 60 inajengwa na mkandarasi China Road and Bridge Cooperation (CRBC) ya jijini Dar es salaam chini ya usimamizi TECU.