Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali mkoani humo kuimarisha mshikamano na mahusiano mazuri ili waweze kulinda rasilimali za nchi.
Kagaigai ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 12,2021 wilayani Same wakati akizungumza na watendaji wa vijiji na kata wakati wa semina yenye lengo la kuwakumbusha wajibu wao pamoja na kutambua mipaka ya kazi katika kutekeleza majukumu yao.
"Niseme kwa wale viongozi ambao hawatakuwa na mshikamano katika kulinda rasilimali zetu, tutatumia utaratibu wa CCM ambao wao huwa na kawaida ya kujadiliana.
"Atakayetushinda itabidi tuwe wakali, maana tunataka nchi isonge mbele, hatutaki mtu wa kutukwamisha wala kuturudisha nyuma. Ili tusonge mbele tunahitaji kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano kwa ajili ya kusimamia miradi ya maendeleo ambayo iko mbele yetu," amesema RC Kagaigai.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoani humo, Jonathan Mabihya amesema ili ushirikiano uwepo baina ya viongozi na viongozi ni lazima waheshimiane ili waweze kutekeleza yale ambayo serikali imedhamiria kufanya kwa wananchi.
"Viongozi msiwe sehemu ya watu wanaopinga maendeleo ni lazima tuwe na ushirikiano katika maamuzi ya pamoja ili tuweze kutekeleza kwa umoja wetu miradi ya maendeleo ambayo serikali imepanga kufanya kwa wananchi," amesema Mabihya.