Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Ibuge kazungumza na wanaopandisha bei vifaa vya ujenzi

17bbabef23d2a0eb00e4a8b33690d5bf.jpeg RC Ibuge kazungumza na wanaopandisha bei vifaa vya ujenzi

Sun, 28 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Wilbert Ibuge amewataka wafanyabiashara mkoani humo kutopandisha bei ya vifaa vya ujenzi wakati huu ambao serikali inaendelea kujenga vyumba vya madarasa na miradi mingine ya maendeleo.

Ibuge alitoa kauli hiyo jana wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayojengwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo ya ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 katika shule mbalimbali za sekondari katika Manispaa ya Songea. Alisema baadhi ya wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, wameanza kuongeza bei hasa ya saruji na kuwataka kuuza kwa bei rafiki ambayo itawezesha miradi inayotekelezwa kukamilika kwa muda uliopangwa.

Aliwaomba kuwa wazalendo na kuepuka kuuza vifaa kwa bei ya juu badala yake, waisaidie serikali kufanikisha mpango huo ambao unakwenda kuwanusuru vijana wasibaki nyumbani kwa kukosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Ibuge aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya za mkoa huo, kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika maeneo yao na viwe vimekamilika kabla ya Desemba 15, mwaka huu.

Aidha, alizitaka kamati za ujenzi kuhakikisha zinakuwa na uadilifu, kuzingatia weledi na uwazi katika shughuli zote ili miradi hiyo iwe yenye viwango na ubora wa hali ya juu na ilingane na thamani ya fedha zilizotolewa. Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisema changamoto katika utekelezaji wa miradi ya vyumba vya madarasa ni kupanda holela kwa bei ya vifaa vya ujenzi, hata hivyo ameahidi miradi yote itakamilika kwa wakati.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Dk Frederick Sagamiko alisema wamepokea jumla la Sh bilioni mbili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu na afya. Alisema fedha kwa ajili ya elimu ya sekondari ni Sh milioni 732.5 kati ya hizo za Covid-19 ni Sh milioni 520 na fedha zilizotolewa na Serikali Kuu ni Sh milioni 212.5. Sagamiko alisema kwa upande wa elimu ya msingi jumla ya fedha zilizotolewa ni Sh milioni 332.5 na kati ya hizo, Sh milioni 140 ni za Covid-19.

Serikali kuu imetoa Sh milioni 112.5 na fedha za TEA ni Sh milioni 80. Kwa upande wa sekta ya afya, Sagamiko alisema fedha zilizotolewa hadi sasa ni Sh bilioni moja ambazo kati yake, Sh milioni 850 zimetolewa na serikali kuu na Sh milioni 160 ni mapato ya ndani ya Manispaa ya Songea.

Chanzo: www.habarileo.co.tz