Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Ibuge ageukia migogoro ya ardhi

IBUGE ED RC Ibuge ageukia migogoro ya ardhi

Sat, 17 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

Jenerali Ibuge alitoa maagizo hayo jana katika kikao kazi cha watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Ruvuma ambacho kilishirikisha watendaji mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala wa wilaya na watumishi wengine ngazi ya wilaya na mkoa kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Alisema maofisa ardhi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kazi, kutojiuhusisha kuomba na kupokea rushwa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria mbalimbali za ardhi.

“Ikumbukwe kuwa baadhi ya migogoro ya ardhi hutokea kutokana na wananchi kutofahamu sheria za ardhi. Kwa hiyo kinachohitajika hapa ni uelewa wa sheria ili wananchi kuzifahamu,” alisisitiza.

Pia aliwataka maofisa hao kuendelea kukamilisha kazi zote za urasimishaji wa makazi holela katika halmashauri zote za mkoa na kwamba kipaumbele kiwe katika Manispaa ya Songea ambako kazi hiyo inafanyika kwa kasi ndogo kulinganisha na wingi wa maeneo yaliyojengwa holela.

Katika hatua nyingine, Jenerali Ibuge aliwataka wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya uwekezaji na yanahitaji fidia, kuendelea kuwa watulivu wakati serikali inatafuta fedha.

Maeneo yanayohitaji fidia yaliyoko Manispaa ya Songea ni Bonde la Mto Ruhila, eneo la EPZA Kata ya Mwengemshindo na Barabara ya By Pass ya Mtwara Corridor.

Katika kikao kazi hicho, RC Ibuge aliwaagiza wanasheria wa halmashauri zote kwa kushirikiana na maofisa ardhi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoa elimu ya namna bora ya kusuluhisha migogoro ya ardhi kwa wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata kwa sababu wameonekana kuwa sehemu ya kikwazo katika kutenda haki kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema, alishauri kuwa ili kutatua migogoro ya ardhi, bajeti ya kupima ardhi iongezwe ili eneo kubwa lipimwe kuepusha matatizo ambayo yanatokana na maeneo mengi kutopimwa.

Chanzo: ippmedia.com