Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Homera avunja ndoa ya manafunzi Mbeya

RC Homera Avunja Ndoa Ya Manafunzi Mbeya Kamanda wa Polosi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga akionesha ng'ombe na mbuzi ambao wametolewa mahari

Fri, 28 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amevunja ndoa ya Juma Mwaigaga, iliyokuwa afunge na mwanafunzi wa kidato cha nne huko Mbeya vijiji.

Imeelezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alikuwa amepata tatizo la kinidhamu shuleni hapo tangu Julai 18, ambapo mwalimu wa nidhamu aliweza kulishughulikia japo inadaiwa kuwa baada ya siku mbili alipotea shuleni hapo.

Hata hivyo baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Majaliwa Amiston amesema alipewa taarifa za kutoonekana kwa binti yake na wanafunzi waliokuwa wakiishi naye hosteli.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, baada ya taarifa hizo, aliripoti tukio hilo ofisi ya Serikali ya kijiji na shuleni pia kisha akaanza ufuatiliaji.

"Nilipofika shuleni mwalimu mmoja akaniambia nisisambaze sana taarifa badala yake nimtafute kimyakimya, ambapo baadaye niliona ujumbe kwenye simu ukisema...niko naye nimemuoa, nikashtuka,” amesema Amiston na kuongeza;

“Ghafla ukaja ujumbe mwingine tena kuwa nakuja huko nimeolewa, kweli wakafika nikaweka mtego Polisi wakawazingira wakawakamata wakiwa na mahari Sh110, 000, Ng'ombe, Mbuzi, Blanketi na shuka na wala sikuvipokea."

Akizungumza wakati wa tukio hilo katika kituo cha Polisi mji mdogo wa Mbalizi wilayani humo, Homera ameagiza Jeshi la Polisi kumsaka Mwaigaga, lakini kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika katika njama za kumuozesha kijana huyo wakiwamo wazazi wake na washenga.

Amesema kuwa kitendo hicho ni unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji na kutamka kwamba licha ya mwanafunzi huyo kueleza awali kuwa hataki kurudi shule, lakini baadaye alisema anataka kurejea tena kuendelea na masomo.

"Imebaki miezi miwili mwanafunzi huyu amalize shule, hivyo amekatishiwa ndoto zake ila kabadili kauli kuwa anataka kurudi shule, hivyo asaidiwe kisaikolojia, vipimo pia vitumike kujua afya yake,” amesema Homera na kuongeza;

"Wazazi wa huyo kijana (Juma), hawa washenga wote wakachukuliwe hatua, huu ni ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia, lakini pia halmashauri jengeni mabweni kwa ajili ya wanafunzi.”

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema tayari watu watatu wamekamatwa, huku jeshi hilo likiendelea kumsaka Mwaigaga kwa tuhuma hizo ili sheria ichukue mkondo wake.

Amewataja waliokamatwa kuwa ni Nazareth Ndele (50), Steven Mwaigaga (29) na Faraja Mwaigaga (26) wote wakazi wa kijiji cha Ikunda wilayani humo, Mkoa wa Mbeya, kwa kuhusika kwenye njama za kumtorosha mwanafunzi huyo kwa lengo la kumuozesha.

"Wapo baadhi ya wazazi wanaoshirikiana na watoto wao wakiwamo wanafunzi kuwashawishi kuwaozesha, lakini tuwashukuru wananchi wanaotupa ushirikiano kufichua taarifa hizi za kikatili na zinazoharibu ndoto za watoto, jeshi la Polisi litawakamata wote waliohusika" amesema Kuzaga.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Eliud Sanga, amesema kiujumla binti huyo hakuwahi kuwa na tabia mbaya wala kuonekana na dalili zozote za utovu wa nidhamu, na kwamba kitaaluma ni mtu wa wastani.

Mmoja wa washenga ambao walifika kukadhi mahari hiyo, Nazareth Ndele, amesema kabla ya tukio Juma alimuomba kupeleka zawadi na mahari ukweni, japo hakuwa anajua kama anayeolewa alikuwa mwanafunzi.

"Mimi sikujua kwa sababu ni jirani yangu na alikuja kuniomba akanipa Ng'ombe na Mbuzi tukiwa watatu na tulipofika ndio tukakamatwa na Polisi hadi kufikishwa hapa," amesema Ndele.

Chanzo: Mwananchi