Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Homera aonya wanaochepuka

Homera Web RC Homera aonya wanaochepuka

Wed, 1 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Juma Homera amekemea vitendo vya baadhi ya wanandoa kutokuwa waaminifu na kufanya mapenzi nje ya mahusiano jambo linalosababisha kuwepo kwa matukio ya mauaji.

Akizungumza jana Jumanne, Februari 28, 2023 ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya Mkoa kuadhimisha kilele cha siku ya Mwanamke duniani ambacho inatarajia kufanyia Machi 8, 2023 katika Wilaya ya Rungwe mkoani hapa.

“Kumekuwepo kwa matukio ya mauaji nchini ambayo yanachangiwa na usaliti katika ndoa na mahusiano ya kimapenzi hali ambayo imekuwa inachocheo matukio ya mauaji dhidi ya wanawake nchini,” amesema.

Amesema ufike wakati wanaume kuwa na hofu ya Mungu kwa kuondoa roho za ukatili dhidi ya wanawake ikiwepo kutafuta suluhu ya migogoro kabla ya majanga kujitokeza.

“Ni kweli mke au mume akichepuka roho inauma, ni jambo la kulitafakari inapojitokeza migogoro ya wanandoa kwa kuchukua hatua ikiwepo kukaa vikao na familia kuzungumza na kutafuta suruhisho,” amesema Homera.

Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza miongoni mwa watu ambao wameathirika na matukio hayo ni wanawake na watoto na kwamba maadhimisho hayo yatumike kukemea matukio hayo ili kuokoa maisha ya kundi hilo nchini.

“Kauli mbiu ya siku ya Mwanamke ni “Ubunifu na teknolojia ni chachu katika kuleta usawa na ufanisi kwa wanawake nchini,” ambayo imetekelezwa kwa vitendo na Serikali ikiwepo uwezeswaji kiuchumi kwa wanawake kupitia asilimia 10 ya mikopo ya halmashauri,” amesema.

Amesema kwa kipindi cha 2021/22 zaidi ya Sh 2.9 bilioni zimetolewa mikopo kwa vikundi 139 katika halmashauri zote za mkoa wa Mbeya ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa kipindi cha Januari 2023 zaidi ya Sh 1.7 bilioni zimetolewa mikopo kwa vikundi 36 vya wanawake, vijana na watu wenye ulamavu lengo ni kuona wanajiajiri kwa kuanzisha miradi endelevu ya kujikwamua kiuchumi,” amesema

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya, Aika Temu amesema maadhimisho hayo yatafanyika kimkoa katika stendi ya mabasi wilayani Rungwe yenye lengo la kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Pia tutatoa elimu ya ukatili dhidi ya wanawake walio katika mahusiano ya kimapenzi na ndoa na changamoto kubwa ni vitendo vya kusalitiana kutokana na kuchepuka.

Neema Joel, Mkazi wa Simile amesema siku hiyo ikatumike pia kufanya usuluhishi wa migogoro katika ndoa kwani imekuwa kiini cha kuibuka kwa matukio ya mauaji dhidi ya wanawake na watoto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live