Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Hapi kufanya ziara ya siku 18 kuijenga ‘Iringa mpya’

11897 Pic+hapi TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilolo. Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi anatarajia kufanya ziara ya siku 18 kuijenga ‘Iringa mpya’ katika wilaya zote na tarafa zake.

Katika ziara hiyo atazunguka kusikiliza kero za wananchi na kupata nafasi ya kuuliza maswali yatakayojibiwa na watumishi wa idara za mkoa huo.

Hapi ameyasema hayo leo Agosti 14, wakati akifanya ziara yake ya kwanza katika wilaya ya Kilolo na kuzungumza na watumishi na watendaji pamoja na wazee wa wilaya hiyo.

Amesema katika siku hizo atazunguka tarafa kwa tarafa kukagua miradi ya maendeleo, viwanda, mashamba na miradi ya umwagiliaji.

“Kwa kufanya hivyo tutawajua watumishi wanaofanya kazi na wasiofanya kazi, kupitia mikutano hii ya tarafa nitasikiliza kero za wananchi na watapata nafasi ya kuuliza maswali na watakaojibu maswali ya wananchi si mimi mkuu wa mkoa, bali watajibu watumishi kulingana na idara zao,”amesema Hapi

Amesema kuwa falsafa yake ni kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe kulingana na utendaji wake wa kazi, kwa kufanya hivyo tutawajua wanaofanya kazi na wanaotengeneza chuki kwa Serikali.

“Nimeletwa Iringa kwa lengo maalumu la kuleta maendeleo na kuijenga Iringa mpya na nitahakikisha nahakiki makaratasi tunayoletewa mezani ili tujue hali halisi kama inaendana na makaratasi tunayopewa na watendaji na wakuu wa idara," amesema Hapi

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Kilolo, mkuu wa wilaya hiyo, Asia Abdallah amesema watendaji wa wilaya hiyo ni watiifu na wanafanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanatimiza majukumu yao vyema.

"Watumishi ni waadilifu kwa nafasi zao na ni watunzaji wa siri za ofisi hivyo nitahakikisha wanashiriki kufanya kazi kwa weledi na wanawasikiliza wananchi," amesema Asia.

Chanzo: mwananchi.co.tz