Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Hapi azuia likizo za watendaji wake, atoa siku 30 wajibu hoja za CAG

27309 Happy+pic TanzaniaWeb

Sat, 17 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amezuia likizo za watendaji wakuu wa halmashauri tano za mkoa huo, huku akiwapa siku 30 kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG).

Wakati halmashauri ya manispaa ya Iringa ina hoja 23 ambazo hazijafungwa, Hapi amesema halmashauri ya wilaya ya Iringa ina hoja 18, Kilolo 16, Mufindi 13 na Mafinga Mji 20.

Aliyasema hayo leo katika ukumbi wa VETA mjini Iringa wakati akifungua kikao chake na watendaji hao kilicholenga kuzijadili hoja hizo na kuweka mikakati ya kuzimaliza ili zifungwe.

 “Jambo hili halileti picha nzuri, kwa nini takwimu zetu mbaya na kwa nini hatuzifanyii kazi hoja hizo ambazo baadhi yake ni za miaka ya fedha iliyopita?” alihoji Hapi.

Hoja hizo zinahusu mapato na matumizi ya halmashauri hizo na utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ikiwamo inayolenga kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

“Likizo zote za kuanzia mwezi huu zimesimamishwa. Hakuna mkurugenzi wa halmashauri au mkuu wa idara atakayepewa likizo ili washughulikie mzigo mkubwa wa kujibu hoja zao za ukaguzi,” amelima.

Pamoja na watendaji hao, Hapi alisema wakuu wa wilaya za mkoa huo nao hawatapewa likizo kwakuwa wana wajibu wa kusimamia utekelezaji wa agizo lake kwa halmashauri zilizo chini yao.

Alisema hayupo tayari kuona Waziri Mkuu Kassim Majliwa akitumwa mkoani kwake kushughulikia kazi inayotakiwa kufanywa na watu waliopewa dhamana hiyo.

 “Kama mnasubiri waziri mkuu atumwe ili yaje yatokee yale yaliyotokea Dar es Salaam hivi karibuni, mie sipo tayari,” alisema akimaanisha yaliyomtokea Dk Charles Tizeba na Charles Mwijage.

Dk Tizeba na Mwijage walitupwa nje ya Baraza la Mawaziri kwa kile kilichoelezwa na Rais John Magufuli kwamba majukumu ya wawili hao katika kushughulikia suala la korosho yalikuwa yakifanywa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Hamid Njovu alisema wamekwishaanza kujibu hoja hizo na kati ya 23 walizokuwa nazo, tano zimejadiliwa na kufungwa na sasa wamebakiwa na hoja 18.

 “Hoja hizo ni za mifumo ya ukusanyaji mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, masurufu yaliyorejeshwa, mikopo ya wanawake na vijana na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema.

Naye mkurugenzi wa Mafinga Mji, Saada Mwaruka alisema katika hoja 20, hoja 11 zimefanyiwa kazi na kufungwa na tisa zilizobaki zinahusu ukamilishaji wa majengo, manunuzi ngazi ya shule, nyaraka za fedha katika ngazi za vijiji na usimamizi wa fedha wa ndani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mufindi, Isaya Mbenje alisema kati ya hoja 15, saba zimekwishafanyiwa kazi na nane zilizobaki zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya alisema kati ya hoja 18 tayari 10 zimejibiwa, Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Josephat Kayombo alisema kati ya hoja 16, hoja nane zimekwishajibiwa na kufungwa.

 Wote kwa pamoja wamekubali kutii agizo la mkuu wa mkoa la kutochukua likizo, wakurugenzi hao waliahidi kujibu hoja zote kabla ya Desemba 15.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz