Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Hapi atoa saa 48 kusafirishwa nguzo

38364 Hapi+pic RC Hapi atoa saa 48 kusafirishwa nguzo

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Wakati wamiliki wa kampuni zinazosafirisha nguzo za umeme wakiendelea na mgomo, mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewapa saa 48 kuruhusu magari yaliyozuiwa viwandani kwa madai ya kusubiri suluhu ya mgogoro wa tozo.

Hapi alitoa agizo hilo jana kwenye kikao na wazalishaji nguzo za umeme, ambao siku za karibuni wameingia mgogoro na Serikali kuhusiana na tozo ya asilimia tano inayopaswa kulipwa kama ushuru wa halmashauri.

Awali, kampuni hizo zilikuwa zikilipa Sh5,000 kwa nguzo badala ya asilimia tano kulingana na matakwa ya sheria.

Hapi alisema magari yaliyopo viwandani yalipiwe na kuanza kusambaza nguzo kwenye miradi inayojengwa maeneo mbalimbali nchini, huku wakurugenzi watendaji wakiendelea kukokotoa hesabu za nyuma zinazotakiwa kulipwa.

“Nimewaomba nimewabembeleza lakini mmekataa kulipa kwa hiari sasa hakutakuwa na kupeana muda wa kulipa wala kikao kingine zaidi ya hiki,” alisema Hapi na kuongeza:

“Mnachotakiwa ni kulipa kumaliza madeni yenu mpaka Jumatatu, kampuni zote ziwe zimelipa au kupunguza madeni.”

Naye mkurugenzi wa kampuni ya New Forest, Lawrence Masha alisema baada ya amri ya mkuu wa mkoa tayari wamelipa Sh61 milioni.

Masha alimuomba radhi mkuu huyo wa mkoa kwa mambo yaliyotokea juzi katika kampuni hiyo na kwamba, yeye hakuwa na taarifa rasmi ya kiwango wanachodaiwa.

“Naomba radhi kwa niaba ya kampuni kutokana na majibu aliyoyatoa mfanyakazi mwenzangu lakini tayari tumelipa Sh61 milioni tulizoandikiwa na mkurugenzi, hesabu zinaendelea kuhakikiwa ili tumalizie deni,” alisema.

Mgogoro huo uliibuliwa na halmashauri ya wilaya ya Kilolo miezi michache iliyopita baada ya mkurugenzi wake kuiandikia barua kampuni ya New Forest kuitaka kulipa asilimia tano ya bei ya nguzo, badala ya Sh5,000.



Chanzo: mwananchi.co.tz