Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Hapi atoa angalizo kwa viongozi wenzake

14696 HAPI+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi amesema viongozi wakikaa ofisini kusubiri ripoti kutoka kwa watendaji wao, wajiandae kupokea uongo.

Amesema hayo leo Agosti 30, 2018 alipotembelea makao makuu ya ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Hapi amesema ili kubaini ukweli, kiongozi wa juu ashuke hadi kwa wananchi wa chini kujua kero zao.

“Tukikaa ofisini tunadanganywa sana, wale tunaoamini ni watendaji kutokana na taarifa wanazotupatia inawezekana ndio wanaolalamikiwa na wananchi,” amesema Hapi.

Amesema, “Ukikutana na wananchi ana kwa ana kuwasikiliza utabaini vitu vingi na maoni yao yanaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa utendaji badala ya kusubiri kuletewa kero zao ofisini,” amesema Hapi.

Ameshauri vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kuandika habari zinazohusu ziara za viongozi kwa wananchi wa ngazi za chini ambazo zinaibua kero zao.

Mkuu huyo wa mkoa amesema habari hizo zina manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.

Hapi amesema anatarajia kukutana na wananchi mkoani Iringa kwa kufanya ziara kila tarafa ili kufahamu kero zao na kutafuta suluhisho la kudumu.

“Si lazima ziwe kero, nikikutana nao ninaweza kubaini fursa zipo wapi, wanawakwama wapi kuzifikia na kuzifungua kwa ajili yao,” amesema Hapi.

Chanzo: mwananchi.co.tz