Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Hapi apewa siku saba kuomba radhi

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa wamempa siku  saba mkuu wa Mkoa  huo, Ally Hapi kuwaomba radhi baada ya kuwataka nao kuwa na vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo.

Hapi alitoa kauli hiyo jana Jumatatu Mei 27, 2019 wakati akizungumza na watendaji wa Serikali kuhusu ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara.

Aliwataja  waandishi wa habari kama wafanyabiashara  na vibarua wasio rasmi, huku akianisha makundi 53 yanayostahili kupata vitambulisho hivyo.

“Wafanyabiashara ni wengi kuna wapiga debe, wauza nyanya,  mchicha,  wachoma mahindi na hata waandishi wa habari na wapiga picha wote wanatakiwa kuwa na vitambulisho ili kuchangia kodi kutokana na kazi wanazofanya,” amesema Hapi.

Akizungumza leo Jumanne Mei 28, 2019 mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Iringa,  Frank Leornald amesema kauli ya Hapi inadhalilisha taaluma ya habari.

Leornald amesema waandishi wa habari mkoani humo wamefanya majadiliano na kuazimia mambo sita watakayoyawasilisha katika ofisi ya mkuu huyo wa Mkoa, na kutaka majibu ya haraka.

Pia Soma

“Tumesikitishwa kuwekwa katika kundi moja linalolinganisha taaluma ya habari na wafanyabiashara. Katika maazimio hayo sita  tumemuomba Hapi kutoa tafsiri rasmi anayoijua yeye kuhusu waandishi rasmi na wasio rasmi.”

“Tunaamini  taaluma ya habari ni kama taaluma nyingine za sheria, udaktari na ualimu hivyo kuingiza wanahabari katika kundi la wafanyabiashara  wanaotakiwa kuwa na hivyo vitambulisho ni kuidhalilisha taaluma yetu,” amesema Leornald.

Amebainisha kuwa Hapi anapaswa kuomba radhi  kutokana na kauli yake hiyo.

“Mengine tutayatolea uamuzi baada ya Hapi kujibu barua yetu tuliyomuandikia,” amesema Leornald.

Leo mchana Mwananchi lilizungumza na Hapi kuhusu kauli yake hiyo na kufafanua kuwa aliwalenga wapiga picha wa mitaani akiwatolea mfano wanaopiga picha watu mbalimbali katika ufukwe wa Coco Beach jijini Dar es Salaam, pamoja na wanaopiga picha katika sherehe mbalimbali.

Chanzo: mwananchi.co.tz