Iringa. Mkuu mpya wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewaeleza watumishi wa mkoa huo kuwa katika utendaji wake wa kazi anaamini katika ukweli, haki na uadilifu.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 6, 2018 wakati akikabidhiwa ofisi na kuwataka watendaji wa Serikali kuwaheshimu wananchi, sheria za nchi na mipaka yao ya kazi.
“Nitasimamia sheria na nitashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na kuhakikisha wananchi hawatoi rushwa ili watatuliwe changamoto zao,” amesema.
Hapi ametaja vipaumbele vyake kuwa ni ulinzi na usalama, kukusanya zaidi mapato kwa kuibua vyanzo vipya, kusikiliza kero za wananchi na kuwashughulikia watumishi watakaozalisha chuki kati ya wananchi na Serikali .
Amesema ataweka utaratibu wa kujitathmini kwa kila mtumishi, kuhakikisha kila halmashauri inatoa asilimia 10 ya mapato yake kukopesha wajasiriamali.
Amebainisha kuwa atahakikisha huduma za jamii zinazidi kuboreshwa na usimamizi wake unakuwa wenye tija.
Hapi amempongeza aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Amina Masenza na katibu tawala aliyeondoka, Wamoja Ayubu kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuleta maendeleo.
Masenza mbali na kumkabidhi ofisi Hapi, alimpa taarifa za maendeleo ya mkoa inayojumuisha mafanikio na changamoto.
Baada ya kukabidhiwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kaimu mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Salim Asas, Hapi alimuagiza katibu tawala kuhakikisha wakuu wa idara zote za Serikali wanakuwa na ilani hiyo, kuisoma na kuitekeleza kulingana na inavyoeleza.